×

COP’s ENEMY’ FILAMU ITAKAYOLETA MAPINDUZI BONGO MUVI

UZINDUZI wa filamu ya Cop’s Enemy uliofanyika jana katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, ambayo iliwashirikisha wasanii nyota kutoka ndani na nje ya Tanzania,  akiwemo Van Vicker kutoka wa Nigeria, Wema Sepetu na Aunt Ezekiel kutoka Tanzania, na kuifanya filamu hiyo kuonyesha uhalisia na utaalam wa hali ya juu, umepongezwa na watu wengi wakisema tasnia ya filamu nchini sasa imepiga hatua

“Hii sasa ndiyo muvi ya uhakika;  ona Wema alivyobeba uhalisia yaani hadi raha kwani  inakufanya uendelee kuiangalia bila kuchoka… Kwa hili wamejitahidi na wanahitaji pongezi,” alisikia shabiki mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Jackie akisema ukumbini hapo.

Mwandaaji wa filamu hiyo, John K-ay, alipozunguza na mwandishi wetu kuhusu filamu hiyo na jinsi ilivyopokelewa, alisema alifurahi kuona Watanzania wengi waliipokea vizuri kazi yake kwa sababu  ni kazi ambayo alikuwa anaamini kabisa  itafanya vizuri na italeta mapinduzi makubwa katika tasnia ya filamu nchini.

“Nafurahi sana kuona Watanzania wengi wananipongeza kwa kazi nzuri niliyofanya.  Niseme tu kwamba huu ni mwanzo, bado nina vitu vizuri kwa ajili yao, naamini hii filamu itaenda kurudisha heshima ya Bongo Muvi, yaani italeta mabadiliko kwenye tasnia yetu, hivyo naomba mnisapoti kwa wingi,” alisema.

Akizungumzia kutokuwepo kwa Van Vicker,  Wema na  Aunt, kwenye uzinduzi huo, alisema waigizaji hao walikuwa na majukumu mengi ya kufanya, na kwamba hata hivyo, hakuna jambo lolote lililoharibika katika hafla hiyo.

“Nilipata taarifa za Wema kuwa anaumwa,  hivyo kwa vyovyote vile asingeweza kufika hapa, lakini Van Vicker ilikuwa ni ngumu kwa yeye kuwa hapa siku ya leo kutokana na majukumu mengi aliyonayo,  na kuhusu Aunt naye ana dharura,” alisema na kuusifia mchango wao ulivyokuwa mkubwa.

Miongoni mwa wasanii waliohudhuria uzinduzi wa filamu hiyo ambayo inapatikana katika @Wemaapp, ni pamoja na Ben Kinyaiya, Lyyn, Ebitoke, Mkali Wenu,  Mzee Kambi, na Senator Msungu.

Na:  Memorise Richard