
WAKATI bado akiwa kwenye presha ya kufukuzwa, kocha mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amefunguka
kuwa haoni dalili za wapinzani wao Simba kuchukua tena ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huku akienda mbali zaidi kwa kusema anajua atamalizia wapi watapokutana.
Simba wanaongoza ligi ikiwa na pointi 18 ikipoteza mchezo mmoja pekee wakati Yanga ipo katika nafasi ya 17 ikiwa
na pointi saba baada ya kucheza mechi nne ikishinda mbili, sare moja huku mchezo mmoja ikipoteza.

Akizungumza na Spoti Xtra nyumbani kwake kabla ya kwenda Misri, Zahera alisema kuwa ana uhakika kwa Simba ya msimu huu haitoweza kuchukua ubingwa licha ya kufanya usajili mkubwa.
“Ligi ya msimu huu ni ngumu kwa kweli, kila timu inajaribu kuonyesha ushindani, binafsi sioni dalili za Simba kutetea ubingwa wao kwa mara tatu, hilo halitowezekana kutokea kwa sababu ukiangalia kila timu inajitahidi kupambana.
“Kushinda mechi nyingi katika ligi ambayo bado haijafika mbali haliwezi kuwa suala ambalo linaweza kuwapa ubingwa kwa sababu huu ni msimu mwingine kila kitu kimebadilika na hata tutakapokutana nao wajue itakuwa tofauti kwani nimeshawajua vizuri mambo yao,” alisema Zahera