
SIKU chache baada ya staa wa Hip Hop Bongo, Ibrahim Mussa ‘Roma Mkatoliki’ kuachia wimbo unaokosoa Serikali wa Naitwa Roma, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, amemkingia kifua mwanamuziki huyo. Awali, baada ya wimbo huo kutoka na kuwa gumzo kila kona, baadhi ya Wabongo walikuwa na hofu kwamba huenda ukafungiwa kwani Roma ameonekana kuikosoa sana Serikali.
Kutokana na hofu ya mashabiki hao, Gazeti la Ijumaa Wikienda lilizungumza na Waziri Mwakyembe ambaye alitoa kauli ambazo zilionesha kumkingia kifua Roma na kusema kuwa hawezi kufungiwa wimbo huo.
“Kuna mambo mengi sana ninayotakiwa kufuatilia na kuyafanyia kazi, hivyo siwezi kushughulika na kila msanii anayetoa wimbo. Kuhusu wimbo wa Roma, siwezi kusema utafungiwa na hata Basata (Baraza la Sanaa la Taifa) nimeshawaambia wasiufungie.
“Wasanii wanaotoa nyimbo ni wengi sana, kwa hiyo siwezi kumfuatilia mmojammoja kwamba ametoa nini, maana unakuta wakati mwingine kuna suala la kuwafuatilia wale wanaokwenda kinyume na maadili kwa kukaa nusu utupu mitandaoni au jukwaani,” alisema Mwakyembe na kuongeza;
“Jamani nchi hii kila mtu ana uhuru wake, umeona kitu anachoandika Zitto (Mbunge Zitto Kabwe) kwenye Mtandao wa Twitter? Mbona hajakamatwa? Tukubaliane tu kwamba Wimbo wa Roma ni wimbo kama zilivyo nyimbo nyingine nyingi.
Ijumaa iliyopita Roma alitoa wimbo unaokwenda kwa jina la Anaitwa Roma aliomshirikisha One Six ambao unakosoa Serikali vilivyo na kuzua hofu kwa mashabiki wake kwamba huenda ukafungiwa.
Baada ya kutoa wimbo huo, habari kutoka kwa mtu wake wa karibu alieleza kuwa Roma hayupo nchini, yupo Marekani kwa hofu ya kwamba huenda akaingia matatani kutokana na wimbo huo. “Roma hayupo Bongo, yupo zake Marekani kwa sababu naye alikuwa anahofia kwamba akiuachia akiwa Bongo, anaweza kuingia matatani,” alisema mtoa habari wetu huyo.
STORI: RICHARD BUKOS NA NEEMA ADRIAN, DAR