Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jafo amewaagiza Wakurugenzi wote nchini wanaotekeleza miradi wa kulipa kulingana na matokeo (EP4R) kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu kuhakikisha hadi kufikia Februari 15, 2020 wanakamilisha miradi hiyo kwa asilimia 100.
Ametoa maagizo hayo leo akati alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Jijini Dodoma.
Jafo amewataka Wakurugenzi wote watakaoshindwa kukamilisha miradi hiyo kwa wakati kuhakikisha wanaandika barua kwa Katibu Mkuu TAMISEMI kueleza kushindwa kutimiza majukumu yao ya kukamilisha miradi hiyo kwa wakati ifikapo Februari 20, 2020.
Amemtaka Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu, Gerard Mweli kuandaa taarifa ya wakurugenzi wote walioshindwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya elimu kupitia mradi wa EP4R na kuiwasilisha kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Mhe. Jafo ifikapo februari, 20 mwakani.
Jafo amefafanua kuwa mara baada ya kupokea taarifa hiyo na kuisoma atatoa mapendekezo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dokta John Pombe Magufuli juu ya Wakurugenzi walioshindwa kutimiza wajibu wao.
“Miradi hii tunaijenga mahususi kwa ajili ya kuwasaidia vijana wetu waweze kusoma katika mazingira mazuri, Serikali imetoa pesa ya kutekeleza miradi hii lakini kuna baadhi ya Wakurugenzi wameshindwa kusimamia utekelezaji wake ambapo fedha zimeisha lakini bado miradi haijakamilisha wakati katika maeneo mengine wametumia fedha hiyo hiyo na majengo yamekamilika kwa viwango,” amesema Mhe. Jafo.
Amewaagiza Wakuu wa Wilaya wote nchini ambapo Miradi ya EP4R inatakelezwa katika Halmashauri zao kuhakikisha wanawasimamia Wakurugenzi ambao wanalegalega katika kusimamia miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na ifikapo tarehe 20 Februari, 2020 wawasilishe taarifa kama Mkurugenzi wake ameshindwa kutekeleza majukumu yake.
Pia, Jafo amewataka TAKUKURU kuchunguza kama upande wa manunuzi kuna shida na kama kulikuwa na mianya ya ubadhilifu wa fedha za Serikali ili wahusika wachukuliwe hatua kwa kukwamisha mradi huu.