
DUNIA inakwenda spidi sana na watu hivyohivyo. Wanakwenda na kasi yake hiyo. Unakuta mtu mzee anafanya mambo ya ujana au ya kitoto. Mwenyewe anaona ni kawaida tu; yaani kwake siyo ishu.
Zamani mwanamke au mwanaume akishafikisha umri wa miaka 50, anakwepa kabisa kufanya mambo yanayoonekana kumvunjia heshima. Alikuwa anajiweka kwenye levo ya utu uzima ili vijana waweze kumuomba ushauri wa kimaisha. Aliaminika kuwa mtu huyo anakuwa na busara na hekima kama Mfalme Suleimani kwenye Biblia.
Kwa sasa mabadiliko ya teknolojia yamekuwa ni makubwa. Yanawaathiri wengi sana. Hofu wala aibu hakuna tena. Ndiyo maana unakuta mama au baba mtu mzima anafanya mambo ambayo hayaendani na umri alionao.
Baada ya kukumbushana kidogo tulikotoka, twende kwenye madhumuni ya makala haya.
Wakati mwaka huu unaelekea ukingoni kabisa, yapo mengi yametokea tangu ulipoanza mpaka sasa. Miongoni mwa yaliyozua gumzo sana na kuweka rekodi ni yale aliyoyafanya mama wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Sanura Kassim almaarufu kama Sandra au Mama Dangote.
Mama huyu amekuwa akifanya mambo mbalimbali ambayo hayaendani na umri wa miaka 50 aliyonayo. Amekuwa akitaka kuonekana kijana zaidi na kusahau kwamba wakati umemtupa mkono; yaani mashavu yameanza kuanguka. Kwa lugha nyingine, jioni imekaribia!
Awali, watu walijua kuwa mama wa mwigizaji, Wema Isaac Sepetu, Mariam Sepetu ndiye mama ‘aliyechangamka’ kuliko wamama wengine wote wa mastaa Bongo, lakini ukweli ni kwamba amezidiwa kete na Mama Dangote.
Yaani Mama Dangote au Mondi ni funika bovu. Amekuwa akijiachia mara ufukweni akiwa amevaa nguo za kuogelea zinazomwonesha maungo yake, mara kujiachia sehemu mbalimbali za starehe bila kujali chochote.
Kama hiyo haitoshi, Mama Mondi amekuwa akijibishana na watu ambao hata siyo wa umri wake kwenye mitandao ya kijamii huku akirushiana vijembe na ‘wakwe zake’, yaani wanawake waliozaa na kutembea na Mondi.
Kiukweli, Mama Dangote kama anavyopenda kujiita, hata kama mwanaye ni staa, lakini anakera baadhi ya watu kwa sababu kama mtu mzima, anatakiwa kujistiri kuliko anayoyafanya sasa.
Yaani skendo za mwanaye Mondi inaonekana hajaziokota popote, bali amerithi kutoka kwa mama yake kwani kama mzazi anafanya kitu kinachofanana na mwanaye ina maana ndiyo tabia yake, hivyo hawezi kumkemea mwanaye kwa namna yoyote.
Kwa mama Dangote ndivyo alivyo kwani familia nzima inafanana kwa matendo. Hakuna wa kumkemea mwenzake kuanzia mama hadi watoto, jambo ambalo linaonesha picha mbaya kwani mzazi hutakiwi kuwa hivyo.
Tabia ya Mama Dangote ya kutupia picha mtandaoni akiwa swimming pool na mumewe Shamte kimahaba wakiwa na nguo za kulalia, imekuwa ikishangaza wengi na kujikuta wakijiuliza inafundisha nini jamii inayomtazama kama mama?
Hivi huwa anajiuliza anafanya hivyo ili amfaidishe nani? Kiukweli inakera na siyo sawa kwa mama kama huyu, anayetakiwa kubadilika.
CHUKUA HIYO
Mama Dangote anatakiwa kubadilika kwa sababu mambo anayoyafanya hayafanani kabisa na umri alionao.
Kama mwaka huu unavyoisha, basi na mambo yako ya aibu unayofanya yaishe na yasivuke mwaka kwenda 2020.
Ukizingatia hili utakuwa na heshima kwa jamii nzima inayokuzunguka. Pia vijana watahitaji sana kupata ushauri kwa kuwa siku zote utu uzima ni dawa!
Makala: Mwandishi Wetu