
KOCHA wa Liverpool, Jurgen Klopp, amemsifu mchezaji wake mpya aliyemsajili hivi karibuni, Takumi Minamino na anaamini staa huyo Mjapan yupo tayari kuanza kuonyesha makali yake mapema kwa timu hiyo inayowania ubingwa wa Premier.
Minamino, 24, alijiunga Liverpool akitokea Red Bull Salzburg kwa dau la pauni milioni 7.25 na atajiunga na wachezaji wenzake wakati dirisha la usajili litakapofunguliwa Januari.
“Taki ni mchezaji ambaye anaweza kutusaidia haraka katika mipango ya muda mfupi na ya muda mrefu. “Ni mzuri sana. Kila mmoja aliona tulipocheza na Salzburg. Lakini bado kuna uwezekano akawa bora zaidi.
“Siyo suala la ushindani, ni suala la kuwa na machaguo tofauti katika mazingira tofauti na mlango uko wazi kwamba Taki anaweza kuingia kwenye timu,” alisema Klopp.
Liverpool ilipata upinzani mkubwa kutoka kwa Manchester United wa kumnasa Minamino lakini mchezaji huyo mwisho wa siku akachagua kwenda Anfield.