
KAMA kawaida ya gazeti lako pendwa la Championi Jumatatu ambalo hukuletea makala za wake wa mastaa mbalimbali ambao wamekuwa wakizungumzia juu ya maisha yao wapi walipoanzia na walipo hivi sasa, leo tumeamua kukuletea mke wa Mzee Ally Samatta, Hadija Omary ambaye ni mama mlezi wa mshambuliaji wa KRC Genk, Mbwana Samatta ambaye anafunguka juu ya maisha yake na mumewe huyo.
Anaanza kwa kusema kuwa: “Nilifunga ndoa na mume wangu miaka tisa iliyopita, mwaka 2011 baada ya yeye kuachana na wake zake wa awali, tulikutania hapahapa Mbagala na kuamua kufunga ndoa.”
UNAZUNGUMZIAJE KUOLEWA FAMILIA YA MPIRA?
“Kwa upande wangu najisikia vizuri kuwa katika familia ya mpira, napata ushirikiano vizuri kama mama na nawatakia kila la kheri wanangu.
JE, UNAISHIJE NA MAJIRANI ZAKO?
“Mimi sipendelei kwenda kwa majirani, siku zote napenda kuzungumza na wanangu na wapangaji wangu tu hapa nyumbani lakini siyo kwenda kwa majirani.
ULIJUA KAMA ALIKUWA MCHEZA MPIRA?
“Wakati naolewa sikuwa nikijua kama mzee Samatta alikuwa mcheza mpira huko nyuma, ila nilikuwa najua watoto wake ndio wacheza mpira ambao ni wanangu.
“Nimejua kuwa mzee Samatta aliwahi kucheza mpira baada ya kufika hapa na kuona picha zake za nyuma alizokuwa akicheza.

UNAZUNGUMZIAJE NAFASI YA SAMATTA KATIKA SOKA?
“Nafurahia mafanikio yake, kwani wakati naolewa yeye alikuwa akiichezea Simba na baada ya hapo akauzwa na kuelekea Congo katika timu ya TP Mazembe na baadaye alifanikiwa kutua Genk ya Ubelgiji.
“Kwa ujumla kama mzazi nafurahia mafanikio ya mwanangu na ninamuombea kwa Mungu aweze kuendelea kusonga mbele zaidi na kupata timu nyingine zaidi.
NINI KILIKUVUTIA KWAKE?
“Mimi mtu mzima na yeye mtu mzima nina miaka zaidi ya 60, hivyo tumeoana, kila mmoja ameridhia kuwa na mwenzie kwa umri tuliofikia.
JE, WATOTO WA MUMEO WANAKUHESHIMU?
“Nashukuru Mungu wanangu wote wananiheshimu kwa kiasi kikubwa mimi mama yao hawaonyeshi tofauti yoyote ninajisikia fahari.
“Kila mtoto amekuwa akinionyesha ukarimu wa hali ya juu, sina shida nao, naishi nao vizuri, siyo kama kina mama wengine. Wananiheshimu vibaya mno.
JE, UMEJAALIWA KUPATA MTOTO?
“Nashukuru Mungu nimejaaliwa kupata mtoto mmoja tu katika maisha yangu anaitwa Dulla anaishi Gongo la Mboto na nina wajukuu watatu, lakini kwa mzee Samatta sijabahatika kupata mtoto hata mmoja.
ALIWAHI KUKUPIGA?
“Hapana na utu uzima huu hajawahi kunipiga wala kunigombeza tunaishi vizuri tu kwa kuheshimiana.
UNAJISHUGHULISHA NA NINI?
“Mimi najishughulisha na kilimo, ni mkulima mzuri, nalima mpunga Malinyi Ifakala huko kwa sasa nipo hapa tunatarajia kwenda kulima kipindi hiki na mwezi wa kwanza tunakwenda kupanda.
“Sijazoea kubweteka hata kidogo licha ya utu uzima wangu, nimezoea kulima tangu nilivyokuwa kwetu, pia nina shamba lingine lipo Vikindu na lenyewe ni shamba la mpunga, hata kama watoto wanatoa msaada ni vyema kuwasaidia kwa kujituma na si kubweteka.”
KHADIJA MNGWAI | Dar es Salaam