
HADI sasa kwenye dirisha dogo, Yanga wamekuwa na kasi kubwa kuliko hata ya upepo wa kisulisuli kutokana na kasi yao ya kushusha nondo katika klabu yao.
Yanga ndiyo timu pekee ambayo hadi sasa imesajili nyota wengi katika dirisha hili dogo ambalo lilifunguliwa Desemba 16, mwaka huu.
Miongoni mwa nyota ambao wamesajiliwa na Yanga ni aliyekuwa straika wa Azam aliyekuwa kwa mkopo Polisi Tanzania, Ditram Nchimbi.
Nchimbi ameletwa ndani ya kikosi hicho maalum kwa ajili ya kuja kuongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji ambalo Yanga iliwatema mastaa wake wa kimataifa akiwemo Juma Balinya na Sadney Urikhob.
Nchimbi alisaini mkataba akiwa Uganda alipokuwa na timu ya taifa, Kilimanjaro Stars kwenye michuano ya Chalenji Cup na kutambulishwa kuwa mchezaji wa timu hiyo.
Mara baada ya kutua rasmi klabuni hapo kama ilivyo kawaida yake Championi Jumatatu, limemtafuta mshambuliaji huyo juu ya klabu yake hiyo mpya na hapa anafunguka kama ifuatavyo.
“Kila siku kuna mambo mapya mengi yanatokea na tunajifunza katika hayo hivyo kwa hatua ambayo nipo kwa sasa kwenye maisha yangu ya soka ni mwendelezo wa kujifunza pia,” anaanza kufafanua Nchimbi.
KWA NINI YANGA?
“Ni moja ya timu kubwa kwenye ardhi ya Tanzania, hakuna mchezaji ambaye hafikirii mambo makubwa, hivyo kuwa kwangu hapa ni moja ya ndoto zangu za muda mrefu ambazo kwa sasa zimetimia.
“Najisikia furaha kuwa hapa. Unajua unapokuwa katika timu nyingine kwa mchezaji ni lazima uwaze kucheza Simba au Yanga na hakuna asiyetamani kucheza katika timu hizo.
HESABU ZAKO ZIPOJE?
“Kama ilivyo sehemu nyingine na hapa nitaendeleza moto wangu, kwani ninaamini katika kipaji changu. Kazi yangu ni mpira, nitacheza kwa juhudi zaidi ya nyuma.
UNAIZUNGUMZIAJE LIGI?
“Ligi ngumu, kila timu inapambana kwa namna ilivyojipanga kufanya vema na kupata matokeo, nyingi zipo kwenye hatari ya kushuka daraja ndiyo maana zinapambana.
“Lakini pia kwa mchezaji kwenye ligi ni lazima uongeze juhudi ili pale ulipokuwepo uongeze ufike mbali zaidi.
UNADHANI UTAENDELEA NA MOTO WAKO?
“Hicho ndicho kilichonileta Yanga, nitapambana kuendelea kuwa kwenye ubora wangu siku zote bila kukoma.
KIPI KIPO NYUMA YA MAFANIKIO YAKO?
“Juhudi katika kile ninachokifanya bila kukata tamaa, kurudia mara kwa mara huku nikiamini kwamba Mungu ndiye mpaji hivyo siachi kufanya na dua pia.
UTAPATAJE NAMBA YANGA?
“Nitaongeza juhudi ya mazoezi yangu, hilo ndiyo nitalifanya kwa ajili ya kupata nafasi hapa.
UNAIONAJE YANGA KIUJUMLA?
“Unajua bado sijaungana na timu lakini pia sijafanya mazoezi na wenzangu, kwa hiyo siwezi kujua sana hali ikoje. Lakini hata pia sijui mifumo ya kocha ikoje hivyo ni suala la muda nikae hapa kisha ndiyo niseme ikoje.
UNAJIPANGAJE SASA NA CHANGAMOTO ZA HAPA?
“Changamoto kila sehemu zipo hata Azam FC, Polisi Tanzania nilipokuwa kulikuwa na changamoto zake. Muhimu ni vile mimi binafsi nitazichukua, nina malengo yangu lakini pia nitajitahidi kujua malengo ya timu ili nifanye kitu kizuri.
YANGA INAKAMIWA SANA, UTAIMUDU PRESHA?
“Bila shaka na hii inaamaanisha kwamba Yanga ni timu kubwa na kila anayetaka kucheza na Yanga naye anataka kuonyesha kwamba anaweza. Kwa hilo halina shida tutapambana kwa kushirikiana na timu kufanya kweli.
UNAHOFIA NINI?
“Namhofia Mungu pekee katika maisha yangu mambo mengine naona ni kawaida tu.
KITU GANI KIGUMU KWENYE SOKA?
“Hakuna ugumu zaidi ya kuelewa kwamba unataka nini na wakati gani ufanye. Ikiwa unajitambua basi kila kitu kinakuwa sawa kwani mpira ni mchezo wa mbinu na akili.
MALENGO YAKO YAPO KWENYE NINI?
“Kuwa mbali zaidi ya hapa, kucheza nje ya Bongo na kufikia hatua za kuwa mchezaji mkubwa na ninaamini huu ni mwanzo kwangu kutoka nje ni suala la kusubiri.
UNAAMINI KATIKA KIPI?
“Katika Mungu, ndiyo maana nipo hapa. Yote yanayotokea ni mwendelezo wa imani yangu katika kazi, namshukuru Mungu kwa kunipigania.
MASHABIKI UNAWAAMBIA NINI?
“Sapoti yao ni kitu cha msingi katika kila mechi na katika kila jambo ambalo tunalifanya kwani sisi bila wao ni hamna kitu. Uzuri wa kile ambacho tunachokifanya kinawahusu wao kwa asilimia kubwa na mafanikio yetu wao wanayabeba.
“Tuombeane dua, watuamini na mimi nitapambana kwa ajili yao.
JANUARI 4 UNAITAZAMAJE NA SIMBA?
“Itakuwa siku nzuri kwangu na timu yetu pia. Wakati ambao tutamenyana na watani wetu Simba, ninaona utakuwa muda bora wa kuonyesha kingine cha kipekee kilichojificha kwenye miguu yangu. Kwa wale wanaobeza uwezo wangu watapata majibu.
“Lakini mechi hii itaonyesha kuwa nastahili kuwepo hapa Yanga au vipi, nitawaonyesha kwa namna gani nimekuwa mkomavu kwa sasa,” anamalizia Nchimbi.
LUNYAMADZO MLYUKA | NA SAID ALLY, Dar es Salaam