×

Undani Mume, Mke Kuchinjwa Kikatili

 

KATAVI: WAKATI Watanzania wakiwa kwenye shamrashamra za kuadhimisha sikukuu ya krismasi, ukatili wa aina yake umeutikisa mkoa wa Katavi baada wa wanandoa Noel Antony Mswanya (39) na mkewe Stela Noel (39) kuuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana na kuzua maswali mengi kwa jamii iliyokuwa inawazunguka.

 

Wanandoa hao ambao ni wakazi wa Mtaa wa Migazini Kata ya Nselwa Manispaa ya Mpanda, waliuawa kikatili kwa kuchomwa na visu na kuchinjwa shingo wakati wakiwa wamelala ndani ya nyumba yao waliokuwa wakiishi pamoja.

 

Ili kupata undani wa tukio hilo la kusikitisha lililoacha majonzi na simamizi kwa wakazi wa Manispaa ya Mpanda, Ijumaa limezungumza na ndugu na viongozi mbalimbali wa eneo hilo ili kupata undani wa tukio hilo lililotokea Disemba 15 mwaka huu.

 

Tukio lilivyokuwa

Akifafanua kwa kina kuhusu tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi; ACP Leonald Makona alisema tukio hilo lilitokea muda wa saa saba usiku katika Mtaa wa Migazini Kata ya Nselwa katika Manispaa ya Mpanda nyumbani kwa wanandoa hao.

 

Alisema kabla ya mauaji hayo, wanandoa hao walikuwa wamelala ndani ya nyumba ndipo wauaji hao walipovunja mlango wa nyumba kwa kutumia jiwe kubwa maarufu kama ‘fatuma’ kisha wakaingia ndani katika chumba walichokuwa wamelala wanandoa hao.

 

“Baada ya kuingia chumbani, walianza kumshambulia marehemu kwa kumchoma na visu katika sehemu mbalimbali za mwili wake huku mkewe akiwa anaangalia licha ya kupiga mayowe ya kuomba msaada kwa majirani, wauaji hao hawakujali.

 

“Baada ya kuwa wamemchinja shingo, wauaji hao ambao hawakufahamika idadi yao, walianza kumshambulia mke wa marehemu. Hata hivyo, aliweza kukimbia nje ya nyumba huku akiwa anapiga mayowe ya kuomba msaada wa majirani.

 

“Wauwaji hao waliamua kuanza kumfukuza mke wa marehemu na kumkamata akiwa umbali wa mita 50 kutoka kwenye nyumba yao na ndipo walimchukua na kumrudisha hadi ndani ya nyumba na kumfanyia mauaji hayo ya kikatili,” alisema kamanda.

 

Aliongeza kuwa majirani waliwashuhudia wauaji hao kwa kuwachungulia kupitia kwenye madirisha ya nyumba zao na waliwaona wakiwa na tochi lakini hakuna jirani hata mmoja aliyefanikiwa kuwatambua wauaji hao.

 

“Majirani wa eneo hilo hawakuweza kutoka nje ya nyumba zao kutoa msaada wakati wa tukio la mauaji hayo kwa kuhofia usalama wa maisha yao,” alisema na kuongeza:

 

“ Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi na msako wa kuwatafuta wauaji hao ili kuweza kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria na tunaomba msaada kwa wananchi waweze kutoa ushirikiano kwa polisi ili watuhumiwa waweze kukamatwa.”

 

Ni ushirikina au kisasi?

Wanandoa hao ambao walizikwa Disemba 17 katika makaburi ya Nsemulwa, mauaji yao yalizusha maswali huku baadhi ya majirani na waombolezaji wakihusisha tukio hilo na kisasi.

Mmoja wa waombolezaji Maria Kilesha, alisema tukio hilo limeacha hofu kubwa kwao kutokana kwa namna lilivyotokea.

 

Alisema watuhumiwa walitumia muda mrefu kutekeleza tukio hilo, bila kuwa na hofu hali inayoashiria wazi kuwa walikuwa wamenuia kufanya jambo hilo kwa kulipiza kisasi.

“Ingawa hatujui kama walikuwa na visasi gani, tunaomba tu vyombo vya ulinzi na usalama kuwa makini muda wote ili kuhakikisha vinadhibiti vitendo hivyo,” alisema.

 

Aidha, John Kaswaya alisema; “Tunaliomba jeshi la polisi liwasake watuhumiwa ili wachukuliwe hatua za kisheria, kitendo walichofanya ni cha kinyama, hata kama ni kulipiza kisasi, hali inatisha…hakika hakitasahaulika kwa wakazi wa mtaa wetu,” alisema.

 

Hata hivyo, jirani wa marehemu hao Everian Steven alisema baada ya kusikia kelele walitoka nje na mumewe na kuwaona watu wamesimama nyumbani kwa marehemu hao.

“Wakaturushia mawe, tukarudi ndani tukitaka kutoka wanarusha mawe kwenye nyumba yetu, muda mfupi kelele hazikusikika tena,” alisema.

 

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Ahamad Bahema alisema tukio hilo ni la kinyama na ni la kwanza kutokea licha ya kuwepo kwa matukio ya wizi yanayotokea mara kwa mara, nimeshuhudia na kutoa taarifa polisi.

Stori: WALTER MGULUCHUMA, Ijumaa

Leave a Comment