×

Mwanafunzi Kidato cha Kwanza Ampa Mimba wa Kidato cha 3

MWANAFUNZI wa kike (17) aliyekuwa anatarajia kuingia kidato cha tatu mwakani katika Shule ya Sekondari Bunambiyu, anadaiwa kupewa ujauzito na mwanafunzi mwenzake ambaye amechaguliwa mwaka huu kuingia kidato cha kwanza mwakani.

 

Mwandishi alifika nyumbani anakoishi mwanafunzi huyo wiki iliyopita na kuonana na wazazi wake. Baba mzazi wa mwanafunzi anayedaiwa kupewa ujauzito, Elisha Mashilimu alisema kuwa kweli mwanawe alibainika kuwa na ujauzito wa miezi mitatu na kufukuzwa shule.

 

Mashilimu alisema kuwa mwanawe alidai kupewa ujauzito na mwanafunzi ambaye amemaliza darasa la saba mwaka huu na amefaulu kuingia kidato cha kwanza. Alisema alikwenda kushtaki polisi na alikamatwa, lakini baadaye walimuona mitaani.

 

“Mimi nimeteseka na mwanangu, lakini binti amekuwa hasemi ukweli, baadhi ya watu wananieleza ujauzito huo si wa mwanafunzi aliyemtaja bali ni kijana mwingine ambaye tumeshindwa kumfahamu, mimi nimechukua jukumu la kumsindikiza kliniki baada ya kuelezwa ana upungufu wa damu, hakuna wa kumtunza, ninawajibika,” alisema Mashilimu.

 

Mashilimu alisema kuwa wazazi wa mwanafunzi aliyetajwa na mwanawe, kuwa kampatia ujauzito walikubali kumtunza na walitoa fedha za matumizi kwa wiki mbili. Baadaye waliacha kutoa na hata kusalimia waliacha, tofauti na ilivyokuwa zamani. Mwanafunzi huyo alipoulizwa aliyempatia ujauzito, alimtaja mwanafunzi mwenzake moja kwa moja kuwa mhusika na kumtaka baba yake achukue hatua ya kuomba fedha za matumizi.

 

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwasubi Kata ya Bunambiyu, Kongezya Kanagano ambako alikuwa akisoma mwanafunzi aliyedaiwa kumpa mimba mwanafunzi mwenzake, alisema kuwa baada ya kusikia tatizo hilo, alimuita anayetuhumiwa kumpa mwenzake ujauzito, lakini alikataa kuwa ujauzito huo ni wake.

 

“Mwalimu naomba nikueleze ukweli, huyu msichana nilikuwa nikimuona na wanaume wengi, mimi ananisingizia sijampa mimba…naombeni mnielewe mwalimu, mimi nakiri sijafanya kitendo hicho, ananisingizia,” alisema mwalimu mkuu.

 

Diwani wa Kata ya Bunambiyu, Richard Sangisangi alisema kuwa habari ya mwanafunzi kupewa mimba na mwanafunzi mwenzake, tena wa shule ya msingi, aliisikia na kushangaa.

 

Alisema alipowauliza wazazi na mhusika, walidai ujauzito ni wa mwanafunzi mwenzake, lakini wakati mwingine wanabadilisha na kumtaja mtu mwingine. Ofisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Joseph Swalala alisema kuwa suala hilo alikuwa hajalisikia, hivyo atalifuatilia ili kufahamu ukweli wake, ikiwa changamoto za mimba wilayani Kishapu zimekuwa ni tishio kwa watoto wa kike. Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba alisema kuwa watoto wa kike, walindwe ili waweze kufikia malengo.

 

Alisema baadhi ya wazazi pande zote mbili, wamekuwa wakimalizana kimyakimya binti anapopata ujauzito. Mwaka huu mimba 56 zimebainika shuleni. Kesi zilizofikishwa mahakamani ni 30 na 26 zinafanyiwa upelelezi.

Stori na Kareny Masasy – Habari LEO

Leave a Comment