×

KMC Yawapa Wanajeshi Dili La Uwanja Wao

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni (KMC), juzi Jumatatu imetiliana saini na Jeshi la Wananchi kikosi cha 361 KJ kilichopo Lugalo jijini Dar es Salaam kuanza rasmi ujenzi wa uwanja wa soka wa manispaa hiyo uliopo Mwenge Dar.

 

Pamoja na uwanja huo unaotarajiwa kuwa wa kisasa, mkataba huo umehusisha ujenzi wa jengo la utawala litakalojengwa Makao Makuu ya Manispaa hiyo, Magomeni, Dar.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta amesema wameamua kuwapa kazi hiyo wanajeshi kutokana na kutokuwa na rekodi ya kuwaangusha kila walipowapa kazi.

 

“Mara nyingi tumekuwa tukiwatumia ndugu zetu hawa katika kazi mbalimbali za kimaendeleo katika manispaa yetu na hakuna siku ambayo wamewahi kutuangusha.

 

“Hivyo naamini hata katika hili la ujenzi hawatatuangusha,” alisema Sitta.

 

Naye msimamizi wa ujenzi huo kutoka kikosi hicho, Luteni Kanali David Michael Luoga, amesema ujenzi huo utaanza hivi karibuni na kukamilika mapema iwezekanavyo na kuiomba manispaa hiyo kuwasilisha vifaa vya ujenzi huo kwa wakati.

 

“Kama mkituletea vifaa vya ujenzi huo kwa wakati tutahakikisha uwanja huo unakamilika ndani ya miezi sita, hivyo naiomba manispaa kuleta vifaa vinavyohitajika kwa wakati,” alisema Luteni Kanali Luoga.

 

Leave a Comment