×

Morrison Ashusha Mghana Mpya Yanga

MUDA si mrefu Yanga itafaidi zaidi matunda ya kiungo wao mshambuliaji raia wa Ghana, Bernard Morrison, hiyo ni baada ya kuwafanyia mchakato wa kumpata straika mpya kutoka Ghana.

Straika huyo anayejulikana kwa jina la Ronald Cobbinah, anatarajiwa kusajiliwa rasmi na Yanga katika usajili ujao wa dirisha kubwa.

 

Morrison ambaye amejiunga na Yanga kwenye usajili wa dirisha dogo uliofungwa Januari 15, mwaka huu, tayari ameonyesha kuaminiwa kwa kiasi kikubwa ndani ya timu hiyo kutokana na ufundi wake wa kuchezea mpira awapo uwanjani.

 

Kabla ya mechi ya jana dhidi ya Prisons, Morrison alikuwa ameichezea Yanga mechi tano za michuano yote na kufunga mabao matatu huku akitoa asisti mbili.

 

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya timu hiyo, kimelinyetishia Spoti Xtra kuwa, baada ya Morrison kutua na kuangalia safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, alilazimika kuushawishi uongozi kumshusha Cobbinah ambaye atakuwa msaada mkubwa kwenye eneo hilo.

 

“Kuna straika mmoja anaitwa Ronald Cobbinah, huyu jamaa ni bonge la mchezaji, Morrison anamfahamu vizuri kwani wamecheza pamoja huko kwao Ghana.

 

“Kuna mpango unafanyika ili katika usajili wa dirisha kubwa ajiunge na timu yetu kuimarisha zaidi safu ya ushambuliaji,” kilisema chanzo hicho.

Spoti Xtra baada ya kuzipata habari hizo, lililazimika kumuuliza Morrison kama kweli anamfahamu straika huyo ambapo alisema: “Ndiyo ninamfahamu, huyo ni ndugu yangu kutoka Ghana, ni mchezaji mzuri tu ambaye akija ataisaidia timu.”

Stori: MUSA MATEJA, Dar es Salaam

Leave a Comment