
KOCHA wa Simba, Sven Vandenbroeck, amefunguka kuwa amekoshwa na uwezo wa kipa wake Aishi Manula na mabeki wake kutokana na kucheza kwa dakika 180 bila ya kuruhusu bao lolote.
Kocha huyo raia wa Ubelgiji, ameweka bayana kwamba, kitendo cha kumaliza mechi dhidi ya Mtibwa Sugar na Lipuli FC bila ya kuruhusu kufungwa ni kitu kizuri kwa upande wao kutokana na kila mmoja kuifanya kazi yake ipasavyo.
Simba katika michezo hiyo, iliifunga Mtibwa Sugar mabao 3-0 ugenini kisha Lipuli FC bao 1-0 juzi. Mechi zote hizo alidaka Manula.
Mbelgiji huyo ameliambia Championi Jumatatu, kuwa kwake anafurahishwa na rekodi hiyo ya kupata clean sheet (mechi bila kuruhusu bao) mbili mfululizo kutokana na kuonyesha wanafanya kazi yao inavyotakiwa.
“Ni kitu kizuri kumaliza mechi ukiwa haujafungwa, inaonyesha kazi ambayo mmeifanya kama timu kuanzia kipa, mabeki na kila mmoja aliye uwanjani.
“Tulishakuwa na clean sheet nne kabla ya Krismasi na kabla ya kuzipata hizi mbili mfululizo. Nafurahia kuona tunashinda mechi ngumu bila ya kufungwa jambo ambalo linatoa taswira kwamba kila mmoja anafanya kazi yake inavyotakiwa kwenye idara yake,” alisema Sven.
Stori na SAID ALLY, GPL

