×

Ronaldo Anamlipa Mpenzi Wake Sh Mil 236 kwa Mwezi

SUPASTAA Cristiano Ronaldo, amekuwa akimpa mchumba wake Georgina Rodriguez dola 80,000 (zaidi ya Sh milioni 236.4) kila mwezi ili kumsaidia kuishi maisha ya kifahari ayatakayo.

 

Mreno huyo pamoja na Georgina, wamekuwa wakiishi maisha ya starehe jijini Turin huku Ronaldo akikomba mshahara wa pauni milioni 28 (Sh bilioni 83 na ushee) kwa mwaka pale Juventus.

 

Wapenzi hawa wana mtoto mmoja waliyezaa pamoja, binti aitwaye Alana Martina mwenye umri wa miaka miwili lakini mrembo huyo pia anawakuza watoto wengine watatu wa Ronaldo.

 

Akiwa ni mama wa nyumbani, gazeti maarufu la Italia, Corriere dello Sport, limedai kuwa Ronaldo anafurahia kumpa mrembo huyo, 26, mkwanja mrefu kila mwezi kwa kuwa pia amekuwa akiwalea watoto wake wengine watatu; mapacha waliopatikana kwa kupandikiza mbegu, Eva na Mateo, pamoja na Cristiano Jr.

 

Huku mamilioni ya fedha yakiingia kwenye familia hiyo kila mwezi, haishangazi kusikia akimlipa mwandani wake huyo kikita kikubwa ili ajirushe anavyoweza huku wakiishi maisha ya starehe.

 

Siku za mapumziko, wamekuwa wakitumia kwenye boti za gharama kubwa huku bethdei zao zikitawaliwa na zawadi za gharama kubwa.

 

Siku Ronaldo anasherehekea bethdei yake ya kutimiza miaka 35, Georgina alimpa mpenzi wake huyo gari la kifahari aina ya Mercedes G-Wagon ambalo bei yake inaanzia pauni 93,000 (Sh milioni 275).

 

Wawili hao pia wamekuwa wakivaa vito vya thamani kubwa sana. Hivi karibuni, Ronaldo aliwaonyesha mashabiki wake saa ya Rolex yenye thamani ya pauni 371,000 (Sh bilioni moja na ushee).

 

Lakini Georgina juzikati aliwaonyesha wafuasi wake kwenye Insta pete ya almasi aliyovaa kidoleni yenye thamani ya pauni 775,000 (zaidi ya Sh bilioni 2 na milioni 290).

 

Georgina pia amekuwa akikomba pauni 6,600 (Sh milioni 20) kwa kila post anayotupia Instagram kunadi kampuni kutokana na wafuasi milioni 16.5 alionao katika mtandao huo wa kijamii.

 

Lakini kabla hajakutana na Ronaldo, Georgina hakuwa na fedha za kutanua namna hiyo. Mzaliwa huyo wa kijijini Jaca, Hispania, alizaliwa katika familia ya kimaskini na ndoto zake utotoni ilikuwa ni unenguaji lakini wazazi wake hawakupata fedha za kumpeleka kwenye shule hiyo, hivyo ndoto zake zikahamia kwenye fasheni.

 

Lakini alijikuta akiibukia kwenye kazi ya uhudumu wa hotelini jijini Bristol, England akilipwa pauni 9.50 (Sh elfu 28) kwa saa. Baadaye alikwenda Hispania kufanya kazi ya kuuza kwenye supamaketi, huko ndiko alikokutana na Ronaldo na maisha yake yakabadilika.

TURIN, Italia

Leave a Comment