×

Wawa: Kisiki cha Simba Kinachoipigia Hesabu Yanga Namna Hii

MIONGONI mwa mabeki visiki ndani ya Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2019/20, huwezi kuliacha jina la Pascal Wawa, raia wa Ivory Coast anaye kipiga ndani ya Simba.

 

Amefanya kazi kwa ukaribu akiwa na Patrick Aussems ambaye alipigwa chini na Simba na hata ujio wa kocha mpya, Sven Vandenbroeck, bado umempa nafasi ndani ya kikosi cha kwanza, hii inatokana na uwezo wake akiwa uwanjani.

 

Wawa, mbali na kuwa beki, ana pasi moja ya bao aliyoitoa kwa Meddie Kagere, Uwanja wa CCM Kirumba wakati Simba ikishinda mabao 4-1.

 

Championi Jumatatu limezungumza naye mengi kuhusu kiwango chake pamoja na mchezo wao wa watani wa jadi Yanga utakaopigwa Machi 8, Uwanja wa Taifa. Huyu hapa:

 

UGUMU UPO WAPI?

“Kutafuta matokeo ndani ya uwanja na ya kuyalinda pia kwa kuwa ukitangulia kushinda ina maana presha inakuwa kubwa, ukitangulia kufungwa pia presha kwako inakuwa kubwa kwenye kulinda lango ili timu isiongezwe mzigo mwingine wa mabao.

 

MCHEZAJI YUPI UNAYEMKUBALI?

“Nje huko huwa napenda kumfuatilia Eric Bailly anayekipiga Manchester United. Nampenda, anatumia akili na nguvu pia. Mwepesi katika kufanya maamuzi, ninapenda mtindo wake wa maisha ndani ya uwanja.

 

USHINDANI UNAUONAJE KWENYE LIGI?

“Ni mkubwa, naona kila siku zinavyokwenda ndivyo mambo yanazidi kuwa magumu. Ndivyo inavyotakiwa kuwa na ligi ngumu ambayo italeta ushindani. Maana halisi ya ligi yoyote bora ni lazima iwe na ushindani.

 

KWA NINI UNAPENDA KUTUMIA NGUVU NYINGI?

“Mazingira ambayo nitakuwepo ndiyo ambayo yananiongoza nifanye nini na kwa nini. Siyo kila mahali nikiwa uwanjani ni lazima nitumie nguvu nyingi, wakati mwingine akili na mbinu za mpira. Wengi wanadhani ninatumia nguvu nyingi, hapana, ni mbinu na akili vinatawala uwanjani.

 

HESABU ZA UBINGWA ZIPOJE?

“Bado kwa sasa, ili utwae ubingwa maana yake unatakiwa usubiri mpaka mwisho uvune kile ulichokipanda kwa kupata matokeo mazuri. Kwa sasa tunapambana kupata matokeo, ubingwa utakuja baada ya kumaliza kazi ya kupata matokeo uwanjani.

 

HOFU YAKO NI NINI?

“Nahofi a kushindwa kujaribu na kuthubutu nikiwa kazini. Ukiachana na hilo, namuogopa Mungu ndiyo maana kwenye kila jambo ninalofanya ninaanza na sala.

 

KIPI UNAPENDA KUKIFANYA UKIWA PEKE YAKO?

“Mazoezi ni kitu ninachokipenda Mazoezi na timu nyumbani huwa maalumu wa kufanya yangu.

“Yote ninafanya ili kuwa kwenye ubora, muda wote ninapenda kuona kile ambacho ninakifanya asilimia kubwa.

 

AUSSEMS NA SVEN TOFAUTI YAO IPO WAPI?

“Bado sijajua kwa kuwa wote ni walimu wazuri na ninakifuata kile ambacho wananieleza.

 

CHAKULA CHAKO NI KIPI?

“Napenda kula wali na samaki, ujue hapa Bongo kuna vyakula vingi vizuri, napenda kweli. Kwangu samaki iwe ni mchemsho ama wakavu poa tu.

 

MCHEZO ULIOPITA NA YANGA ILIKUWA SARE, MATOKEO HAYA UNAYAZUNGUMZIAJE?

“Ni kama ilivyo kwenye timu nyingine,  matokeo yapo na kinachotokea ndani ya dakika 90 huwezi kukibadili.

 

KUELEKEA MCHEZO WENU, JE HESABU ZIPOJE?

“Mechi zetu zote tunazocheza tunazichukulia kwa uzito sawa, hakuna mechi yenye umuhimu kuliko nyingine, zote kwetu ni muhimu.

 

“Tulishindwa wakati uliopita, unaitazama kwa umuhimu mkubwa kwa kuwa tukishinda tutapata pointi tatu na hicho ndicho tunachokihitaji.

 

UNAKIONA WAPI KIKOSI CHA SIMBA?

“Kwenye hatua kubwa ambayo tumekubaliana kwa pamoja tukiwa ni wachezaji kutimiza majukumu yetu ipasavyo. Simba ni timu kubwa nasi tuna kazi ya kukipeleka kikosi kwenye hatua kubwa zaidi.

 

FURAHA YAKO INABEBWA NA NINI?

“Ushirikiano uliopo ndani ya timu, wachezaji tunashirikiana na kutafuta ushindi kwa pamoja, tukishindwa, tukishinda tunaungana na kuwa wamoja.

 

UKIWA NA HASIRA UNAFANYA NINI?

“Muziki huwa unanifanya nifurahi zaidi na nikishindwa hapo nitafanya mazoezi kila kitu kitakuwa sawa kwani maisha ni lazima yaendelee,” anamalizia Wawa.

MAKALA: LUNYAMADZO MLYUKA, Dar es Salaam

Leave a Comment