KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Sven Vandenbroeck, ametoa onyo kwa wachezaji wote wa timu hiyo akiwemo Luis Miquissone na Clatous Chama kwa kuwataka kucheza soka la pasi nyingi badala ya kukaa na mpira muda mrefu. Simba inayoongoza ligi kwa pointi 62, jana Jumatano ilicheza na Azam katika Uwanja wa Taifa jijini Dar ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Baada ya hapo, Jumapili itacheza dhidi ya Yanga uwanjani hapo ukiwa ni mwendelezo wa ligi hiyo. Akizungumza na Spoti Xtra, Sven alisema kuwa anapendelea kuona zaidi timu yake ikicheza soka la pasi nyingi tofauti na mchezaji mmojammoja kukaa muda mwingi na mpira kwani haiwezi kuwa msaada katika timu.
“Unajua Simba soka la kasi imekuwa kama ndiyo utamaduni wake, nimekuwa nikipenda kuona wachezaji wakicheza hivyo kwa sababu inasaidia zaidi timu kutengeza nafasi na ukiangalia tunapambania ubingwa.
“Lakini unakuta mchezaji anapenda kukaa na mpira muda mwingi kitu ambacho kwangu siyo sawa kutokana na malengo ambayo tupo nayo, tunaenda kucheza na Yanga ambao tunahitaji kupata ushindi, sasa ni kitu bora kuona wachezaji wanatambua majukumu yao,” alisema Sven.

