Watu 82 raia mataifa tofauti wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kosa la kuingia na kuishi nchini huku Mtanzania mmoja akishitakiwa kwa kosa la kumuhifadhi raia wa kigeni kinyume na sheria.
Washitakiwa hao kati yao ni kutoka taifa la Burundi, Malawi, Kenya na Msumbiji ambapo wote wameshitakiwa kwa makosa mawili.
Akiwasomea maelezo ya awali washitakiwa hao, mbele ya Hakimu mkazi wa mahakama hiyo VICKY MWAIKAMBO wakili wa Serikali SITTA SHIJA amedai kuwa raia hao wametenda kosa hilo kati ya tarehe mbili na tatu maeneo tofauti jijini DSM.
Kwa upande wake wakili wa Serikali GODFREY NGWIJO akiwasomea washitakiwa hao mashitaka yao yanayowakabili amedai kuwa, kati ya tarehe mbili na tatu mwaka huu, washitakiwa hao kwa pamoja wakiwa raia wa nchi tofauti wamekamatwa wakiishi nchini bila vibali maalumu vya kuwaruhusu kufanya hivyo.
Aidha wakili NGWOJO mbele ya Hakimu mkazi RASHID CHAUNGU amedai kuwa mtanzania MOHAMED MBISE mkazi wa Manzese jijini DSM anadaiwa kumuhifadhi AMISA NIYONKURU raia wa Burundi kinyume na sheria.
Hata hivyo baada ya kusomewa mashitaka yao nakukiri kosa mahakama hiyo imewaamuru kati ya washitakiwa hao kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya milioni moja kila mmoja na wengine wakitakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya laki tano kila mmoja ama kifungo cha mwaka mmoja Jela.
Baada ya maelezo hayo wakili wa Serikali amedai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 12 na 19 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa wote wamerudishwa rumande.
