MWENYEKITI wa Klabu ya Yanga, Dr Mshindo Msolla amewaambia mashabiki wa timu hiyo ‘Msiogope, Mnyama anakufa mapema tu, huku akiwataka kuwa na mshikamano kuelekea mchezo wa Kariakoo Derby.
Yanga na Simba zitakipiga keshokutwa Jumapili kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara unaosubiria kwa hamu kubwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ikiwa ni raundi ya pili ya ligi hiyo.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Msolla alisema wao kama viongozi wametimiza wajibu wao kuhakikisha wachezaji wanapata kila kitu kwenye maandalizi huku akiwataka mashabiki na wadau wa Yanga kuungana nao katika kuhakikisha wanashinda mchezo huo.
Msolla alisema moja vitu walivyovitimiza ni kuhakikisha timu inakaa kwenye kambi nzuri yenye ulinzi wa kutosha wakihofia hujuma kutoka kwa watani wao.
Aliongeza kuwa ana matarajio makubwa ya kupata ushindi katika mchezo huo kama viongozi na mashabiki wa timu hiyo wataungana kwa pamoja katika kuelekea pambano hilo.
“Kwa upande wetu viongozi, tumejitahidi kutimiza majukumu yetu ili kuhakikisha timu inakuwa na mazingira mazuri. Hivi sasa Tumeweka utaratibu wa kuzungumza na wachezaji pamoja na benchi la ufundi kwa wakati tofauti.
“Huo utaratibu tumeuanza katika kuelekea mchezo wa Simba ambao tutaendelea nao katika michezo mingine ya ligi na kikubwa tunataka kuona timu inapata ushindi kwenye mechi tulizozibakisha.
“Hivyo, niwatake Wanayanga wote hivi sasa kushikamana na siyo kuwaachia viongozi pekee na badala yake kushikamana kwa nafasi na uwezo wake ili kuhakikisha tunashinda mchezo huo,” alisema Msolla.
Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam

