CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), uhai wake umeonekana kuyumba kutokana na wabunge na madiwani wa chama hicho kujiunga na CCM.
Licha ya wabunge na madiwani, vitu vingine vilivyolegeza nguvu ya Chadema, ni kitendo cha mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye kurejea CCM, sambamba na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji.
Lakini pia kitanzi cha zuio la siasa za kuuza sera majukwaani, ikimaanisha mikutano ya hadhara kwa viongozi wao wa kitaifa kupigwa marufuku, ni janga lingine kwao.
Wabunge waliohamia CCM ni Mwita Waitara (Ukonga), Julius Kalanga (Monduli), Chacha Marwa Ryoba (Serengeti), Godwin Mollel (Siha), James Ole Millya (Simanjiro), Pauline Gekul (Babati), Joseph Mkundi (Ukerewe) na Cesil Mwambe (Ndanda).
Pamoja na hali hiyo, bado viongozi waandamizi wa Chadema nao wanakabiliwa na kesi kadhaa mahakamani.
Kutokana na wimbi hilo la misukosuko, ndiyo maana nasema itakuwa imeidhoofisha Chadema ile ya mwaka 2015.
Profesa wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mohamed Bakari anakiri kwamba viashiria hivyo vinaonesha kukiathiri chama hicho kisiasa, japokuwa ni vigumu kutabiri kwa sasa nguvu yake itakuwaje wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
“Kwa sababu kilichofanya wafanikiwe Chadema siyo umadhubuti wa chama, ila kuna wimbi la mabadiliko lililokikumba chama tawala, kwani baadhi ya vigogo wa CCM walihamia upinzani 2015.
“Lakini pia kulikuwa na wimbi la Ukawa ambalo lilikuwa limekubalika sana na wapiga kura, hata mwaka 1995 ilikuwa ni wimbi kwa upinzani,” anasema Profesa huyo.
Anasema upo uwezekano mkubwa kwa chama hicho kudhoofishwa kwa namna moja ama nyingine kama hakitatafuta mbinu mbadala kujinusuru.
“Ila tukumbuke kuwa uchaguzi ni uchaguzi tu, tunaweza fikiri hivi, lakini kikaja kufanya vizuri kwa sababu bado kuna watu wanaotaka mabadiliko. Kwa miezi iliyobakia lolote linaweza kutokea,” anasema mtaalam huyo.
Naye Dk Muhidini Shangwe wa Idara hiyohiyo kutoka UDSM, anakubaliana na mtazamo wa Profesa Bakari akifafanua nadharia yake kuhusu ukimya wa vyama majukwaani, unaweza kutengeneza matamanio makubwa ya kusikika kwa Watanzania kuliko sauti zilizozoeleka kwa sasa majukwaani.
“Wapo wananchi ambao wanatamani kusikia jambo gani Chadema watazungumza kwa mara ya kwanza baada ya kuruhusiwa kufanya siasa majukwaani,” anasema.
Pamoja na fursa hiyo kwa upinzani, Dk Shangwe anatazama siasa za Tanzania zimejengwa katika uwezo wa mwanasiasa mmojammoja zaidi kuliko chama.
“Kwa hiyo nina shaka, Chadema ya mwaka 2015 huenda isitokee tena mwaka huu labda utokee mpasuko CCM,” anatabiri.
Lakini Mkurugenzi wa Itifaki, Uenezi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema anasema pamoja na changamoto hizo, Chadema haijaathiri uhai wake na badala yake imeendelea kujiimarisha.
“Lowassa aliingia na mafuriko ya vigogo Chadema, lakini hakuondoka nao wote kurudi CCM. Sumaye alikuja na kuondoka peke yake, Dk Mashinji ameondoka mwenyewe, sasa unapimaje athari zao?”
Mrema anaongeza kuwa kwa mara ya kwanza chama hicho kilifanikiwa kusimamisha wagombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa zaidi ya asilimia 80 licha ya figisu zilizofanyika na kuamua kujitoa.
“Jambo la tatu ni kwamba licha ya kuzuiliwa kufanya mikutano ya kisiasa, Chadema tumetekeleza program ambayo ni msingi kwa asilimia 100, kwa sasa tuna kiongozi wa chama kila kijiji Tanzania Bara, tunajua wako wapi, namba zao za simu na majina yao, kwa hiyo wapo wanaoondoka na wapo wanaoingia kujenga uhai wa chama, uchaguzi ujao tutakuwa vizuri sana,” anasema Mrema.
“Kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika 2015, aliondoka Katibu Mkuu wa Chadema, Dk, Wilbrod Slaa, lakini Chadema kikaimarika zaidi, kwa hiyo kuondoka kwa baadhi ya watu hakuwezi kukiyumbisha chama,” anasema Mrema.
Kati ya mwaka 2015 hadi Februari, mwaka huu, chama hicho kimepoteza majimbo 12.
Kuhusu mazingira hayo, Mrema anakiri kwamba imekuwa changamoto na doa kwa chama na wapiga kura waliokatishwa tamaa na wanaohamia CCM.
“Lakini tumejipanga kuwa na mchujo, wagombea wote watakaojitokeza tutawaweka katika program maalum ya mafunzo. Baada ya mafunzo hayo, kutakuwa na mchujo chini ya Kamati Kuu ya chama kupitia kanuni za uteuzi za mwaka 2015, zitakazoboreshwa kwa kuzingatia sifa za mgombea, vigezo na masharti yatakayowekwa.”
Lakini Mbunge wa Moshi- Vijijini, Anthony Komu anasema mwanachama kuondoka ni jambo la kawaida.
“Kushindwa Chadema ni kawaida kwa sababu vyama siyo mama yetu, lakini vyama vitaendelea kuwepo, vyama ni mali ya wanachama, wanachama ni roho ya vyama. Niwaambie watu wa Moshi, kama Chadema kutanishinda, nguvu zangu nitazipeleka kwingine kuimarisha upinzani zaidi,” anasema Komu.
Pamoja na tathmini ya wadadisi katika duru za kisiasa, mbinu za chama hicho zikilinganishwa na changamoto zilizojitokeza, wanajiuliza, je, kitarejea katika ushindani kama ilivyokuwa mwaka 2015?
Uchaguzi huo ulijiandikia historia ya uhai wa chama hicho baada ya kupata kura zaidi ya milioni sita za urais chini ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyegombea nafasi ya Urais baada ya kukihama chama chake cha CCM na chama hicho kiliongeza uwakilishi ndani ya Bunge kwa zaidi ya wabunge 30 ikilinganishwa na mwaka 2010.
Na Elvan Stambuli
Simu: 0655-339616
