WAANDISHI wa habari wanne Mkoani Morogoro wameungua moto wakati wakifuatilia tukio la nyumba kuwaka moto katika eneo la Msamvu Mizambarauni, Jirani kidogo na eneo ilipotokea ajali ya lori lililolipuka na kusababisha vifo vya watu 100.
Waandishi hao ni Nicolaus Mwanarusi wa Global Publishers na wengine wa Abood Media, Star TV na Imani Media.
Akizungumza na www.globalpublishers.co.tz, Mwanarusi amesema wakati tukio hilo likitokea, walikuwa kwenye semina, hivyo wakapokea taarifa ya moto huo kutoka kwa wasamaria wema waliokuwa eneo hilo.
“Tulitoka haraka na vifaa vyetu kuwahi eneo la tukio, tulipofika tukakuta nyumba inateketea kwa moto, kwa mujibu wa mashuhuda walisema chanzo ni kulipuka kwa mitungi ya gesi iliyokuwa imetunzwa humo, wakati tunaendelea kuripoti ulilipuka mtungi mwingine uliyokuwa karibu yetu.
“hivyo tukaanza kukimbia kuokoa maisha yetu, wenzetu wawili waliungua na wameumia vibaya ila sisi wengine wawili hatukuumia sana. kwa mfano mimi niliungua kidogo kwenye goti. Sote tumeletwa hapa Hospitali ya mkoa na tunaendelea na matibabu. Tumepoteza baadhi ya vifaa vyetu vya kazi kulingana na hali yenyewe ilivyokuwa wakati wa kujiokoa,” amesema Mwanarusi.
Aidha, Jeshi la Zimamoto limefanikiwa kuuzima moto huo na kuahidi kutoa taarifa kamili ya tukio hilo hapo baadae kidogo.

