BAADA ya Yanga kusimamisha program zake za mazoezi, kiungo wao mnyumbulifu, raia wa Ghana, Bernard Morrison amejiweka kizuizini ili kuepuka maambukizi ya Virusi cya Corona kwa kuhamishia mazoezi yake ufukweni na kukaa ndani kwake muda wote.
Tangu Morrison ajiunge na Yanga, Januari, mwaka huu, ameshafanikiwa kuifungia Yanga mabao matatu pekee huku akiisaidia kupata ushindi kwa kutoa pasi za mabao mawili.
Akizungumza Morrison alisema kutokana na hali ya maambukizi ya Corona, kwa sasa atakuwa akipiga mazoezi ya pekee kwenye fukwe mbalimbali ambazo hazina msongamano, na kisha kurejea nyumbani kwake ili kuepuka kukutana na watu wengi.
“Tangu jana (juzi Jumatano) uongozi wetu ulipotangaza kusitisha mazoezi yetu, nimejikuta nikitafakari na kuamua kununua mahitaji yangu yote na kuweka ndani ili nisipate tena muda wa kutoka na kujichanganya na watu kwani hali ya hewa siyo nzuri na kwamba njia niliyogundua pekee ni kujizuia kabisa kutoka.
“Nimejipangia kuanzia sasa nitakuwa nikitoka kwangu hapa Afrikana (Dar) na kwenda kufanya mazoezi kwenye fukwe za karibu ili niepuke zaidi kupanda gari na kukutana na watu mbalimbali maana huwezi kujua wapi unaweza kukutana na gonjwa hili,” alisema Morrison.
Stori: Musa Mateja, Dar es Salaam

