SIMBA wamewaambia Yanga kwamba: “Kama mnamtaka Clatous Chama na Deo Kanda, njooni fasta tufanye mazungumzo. Hakuna kinachoshindikana.
Kauli hiyo ya Simba imetolewa na mtendaji mkuu, Senzo Mazingisa ikiwa ni siku chache tangu kuwepo kwa taarifa za Yanga kuonyesha nia ya kumuhitaji kiungo wa Simba, Clatous Chama raia wa Zambia pamoja na Deo Kanda raia wa DR Congo.
Yanga kupitia kwa wadhamini wao, Kampuni ya GSM, hivi sasa inataka kuingia sokoni kwa nguvu zote huku ikisema ina uwezo wa kumsajili mchezaji yeyote ambaye anaonekana anafaa kuichezea timu hiyo.
Akizungumza na Spoti Xtra, Senzo alisema kuwa timu yeyote iwe AS Vita, Al Ahly, Mamelodi Sundowns hata Yanga kama inawahitaji Chama na Kanda wanatakiwa kufi ka mezani kwa ajili ya kufanya mazungumzo juu ya wachezaji hao kwani hakuna kitu ambacho kinashindikana kwenye mpira.
“Si Yanga pekee ambao tunawakaribisha mezani kwa ajili ya kufanya mazungumzo kama wanawahitaji wachezaji wetu Chama na Kanda, ila hata AS Vita, Al Ahly na Mamelodi Sundowns tunazikaribisha pia.
“Wachezaji siku zote wapo kama spea tu, leo anaweza akawa hapa na kesho akawa pale, hata sisi tukihitaji wachezaji lazima tukazungumze na timu zao, tukifanikiwa tunamsajili,” alisema bosi huyo raia wa Afrika Kusini akizungumza kwa Lugha ya Kiingereza.
Wakati Simba wakitoa kauli hiyo, Spoti Xtra likamtafuta Ofi sa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz kuzungumzia juu ya usajili wa wachezaji hao wawili ambapo alianza kwa kucheka kisha akatoa kauli ya kibabe kwamba: “Ni suala la muda tu ambao ndiyo utazungumza kila kitu.
”Kwa upande wa Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said, amesema, wanataka kuijenga upya Yanga, hivyo ni lazima walete wachezaji bora zaidi kwenye kikosi hicho.
“Kama tunataka kujenga timu yetu lazima tulete wachezaji bora ambao watakuwa msaada kwetu. Kapteni (Papy Tshishimbi) tumemalizana naye.
“Wachezaji wenye viwango vya juu ndiyo ambao tunawahitaji hapa kama ilivyo kwa Morrison (Bernard),” alisema injinia huyo.Ikumbuke kuwa, Kanda anaichezea Simba kwa mkopo akitokea TP Mazembe ya DR Congo, ambapo mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu, huku Chama mkataba wake ndani ya Simba ukitarajiwa kumalizika 2021.
MARCO MZUMBE NA SAID ALLY, SPOTI XTRA

