WAKATI idadi ya wagonjwa walioambukizwa virusi vya corona imefi kia 147 nchini kote, habari njema ni kwamba 127 kati yao wanaendelea vizuri kwani wanatembea vizuri, wanazungumza na baadhi wameanza kufanya mazoezi.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu alipokuwa anazungumzia mwenendo wa maambukizi ya ugonjwa huo hadi kufikia jana Aprili 17, 2020.
Waziri Ummy alisema wakati idadi sasa imefikia 147, wagonjwa 11 wamepona na kuruhusiwa huku wengine 127 wakiendelea vyema na wanne wakiwa katika hali mbaya. Alisema vipimo vya juzi (Aprili 16) katika Maabara ya Afya ya Jamii vimebaini kuwapo kwa wagonjwa wengine wapya 53.
Aidha alisema kwamba pamoja na kuwapo kwa matumaini makubwa, mgonjwa mwingine amefariki dunia kwa ugonjwa huo na kufanya idadi ya wagonjwa waliokufa hadi sasa kuwa watano.
Aidha alifafanua kwamba wagonjwa wanne ambao wapo katika hali mbaya ni wale ambao wana matatizo mengine ya kiafya. Akichambua zaidi takwimu za wagonjwa wapya alisema Dar es salaam wapo wagonjwa 38 , Zanzibar 10, Kilimanjaro mmoja, Mwanza mmoja, Lindi mmoja, Kagera mmoja na Pwani mmoja.
Kwa upande wa Zanzibar, taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya Zanzibar inasema jumla ya watu 11 wamegundulika kuugua ugonjwa wa corona na kufanya jumla ya wagonjwa walioambukizwa visiwani humo kufikia 35.
Waziri wa Afya wa Zanzibar Hamad Rashid Mohamed alisema walioambukizwa wanatoka sehemu mbalimbali za Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja. Alisema wagonjwa hao wote hawana historia ya kusafiri nje ya nchi na hivyo kumaanisha kwamba maambukizi ya ugonjwa wa corona sasa yamo ndani ya nchi.
“Tumepokea wagonjwa wengine 11 wapya wa ugonjwa wa corona na sasa kufanya idadi ya wagonjwa hao kufikia 35 ambapo maambukizi yote yanatoka ndani ya nchi,” alisema. Wakati huohuo serikali imeagiza Mamlaka ya Hospitali ya Taifa Muhimbili kuacha kupokea wagonjwa wenye dalili za corona.
Aidha imewataka wananchi wanaohisi dalili za corona kwenda katika vituo na maeneo ambayo serikali imeyaelekeza.

