MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Kiongozi Mkuu Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amesema njia kuu ya kisayansi ya kupunguza au kuzuia maambukizi ya Covid-19 ni kuvunja mwingiliano wa watu, “Lock down” japo ni njia ngumu na yenye gharama kubwa za kiuchumi hususani kwa nchi masikini.
Mbowe amesema hayo leo Jumatano, Aprili 29, 2020, Jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia mwenendo wa maambukizi ya ugonjwa wa covid 19 nchini Tanzania.
“Ni ujinga uliopitiliza kwa nchi yoyote kufikiria ina uwezo wa kukabiliana na corona kwa utaratibu wake wa ndani, iwe kwa misingi ya kiuchumi, kisayansi, kitabibu, kiutamaduni, kwa imani za kidini na mbaya zaidi hata kwa imani za kishirikina.
“Ni ujinga zaidi kutokujifunza kwa uzoefu kutoka kwa nchi zilizotangulia kupambana na janga hili la corona, janga hili linahitaji dunia kupambana pamoja kwa kushauriana na kusaidiana. Tunataka mseme ukweli ili dunia ije itusaidie, sisi tunatoa takwimu za uongo,WHO wanatushangaa, tunaficha ukweli kuhusu ugonjwa huu hatari duniani.
“Msishangae kesho nimekamatwa kwa sababu nimesema mambo ya msingi, siko tayari kufa, kuna misiba mingi, kama kuna mtu anadhani ugonjwa wa corona ni utani tunajidanganya.
“Hadi leo tunapozungumza ndugu Watanzania hakuna Bajeti yoyote iliyoidhinishwa na Bunge au Serikali kwa ajili ya kupambana na Corona na Wala Watanzania hawajui Serikali ina mpango gani juu yanamna ya kukabiliana na Corona.
“Tunamtaka Rais Magufuli asione aibu juu ya janga hili la Corona na sijui kwa Nini Rais Magufuli anafanya Siri na hashirikishi wananchi juu ya janga hili la corona. Corona ni janga la Dunia Wala halijazaliwa Tanzania kwa hiyo lisiwe siri,” amesema Mbowe.
