“WAAMBIE nakuja” Hiyo ni kauli ya beki wa kati Mike Kibwage ambaye ni raia wa Kenya akituma ujumbe kwa mashabiki wa Simba kuwa atakuja kuichezea timu yao kama watampa ofa nzuri.
Simba iko kwenye kazi kubwa ya kuhakikisha inasuka safu yake ya ulinzi ambayo Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Sven Vandenbroeck anaonekana kutoridhishwa nayo kwa madai inaruhusu sana mabao.Sasa imekuwa ikitajwa kuwafuatilia mabeki wengi baadhi yao ni Bakari Mwamnyeto wa Coastal Union, Yakubu Mohammed anayekipiga Azam FC na sasa Kibwage anayecheza KCB ya Kenya ameongezeka.
Akizungumza na Championi Jumamosi, moja kwa moja kutoka Kenya, Kibwage anayekipiga KCB inayoshiriki ligi kuu ya nchini humo, ameweka wazi kuwa licha ya kuwa hajafuatwa rasmi ya Simba lakini yuko tayari kutua kikosini humo na kufanya makubwa.
Beki huyo mwenye urefu wa futi sita, aliongeza kuwa kwa sasa ana mkataba ambao unaisha Oktoba, mwaka huu na kama Simba wakipeleka ofa nzuri basi hawezi kukataa na atapiga kazi vizuri tu.
“Nimesikia kuwa Simba wananitaka lakini hawajanifuata rasmi, hata hivyo niko tayari kuja kuichezea timu hiyo kama watakuja na ofa nzuri siwezi kuikataa,” alisema Mike.