×

Kurudi Katika Ubora… Marcelo Ana Kazi ya Kufanya

BEKI wa kushoto wa Real Madrid, Marcelo, tayari amejijengea jina ndani ya klabu hiyo kuwa miongoni mwa nyota waliofanikiwa zaidi.

Akiwa anasherehekea mafanikio yake ndani ya klabu hiyo, Jumanne ya wiki hii alikuwa anatimiza miaka 32 ya kuzaliwa kwake.

 

Marcelo ametwaa mataji tofauti huku akivunja rekodi kadhaa ndani ya Madrid.

Lakini mbali na yote hayo, anakumbwa na changamoto ambazo zinamtesa ndani ya klabu hiyo kwa sasa.

Hapa kuna mambo matano ambayo Mbrazili huyu anakumbana nayo ndani ya Madrid na ana kazi ya ziada ya kufanya.

 

KURUDI KIKOSI CHA KWANZA

Kwa sasa Marcelo anasugua benchi mbele ya Ferland Mendy ambaye ameonekena kumshawishi vilivyo kocha wa kikosi hicho, Zinedine Zidane.

Tangu Marcelo akumbwe na majeraha ya mara kwa mara, nafasi yake kikosini imekuwa finyu sana.

Wakati akiangaliwa katika kuirudisha namba yake, kumekuwa na tetesi kwamba anaweza kuondoka klabu hapo mwishoni mwa msimu huu.

 

KUVUNJA REKODI YA CARLOS

Roberto Carlos ambaye ni Mbrazili mwenzake anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji wa kigeni kuwahi kuitumikia Real Madrid kwa kucheza mechi nyingi ambazo ni 527.

Mpaka sasa, Marcelo amecheza mechi 505 ndani ya Madrid, akifuatiwa na Mfaransa, Karim Benzema aliyecheza mechi 501.

Hapa kuna kazi kwake kuendelea kupambana kuhakikisha anacheza zaidi na Zaidi kuifikia rekodi ya Carlos na kuivunja kabisa.

 

KURUDI KATIKA USHAWISHI

Kwa kifupi, Marcelo hivi sasa hana ushawishi wowote kwa mashabiki wake tangu kuanza kwa msimu huu.

Msimu huu amecheza mechi 19 na kufunga bao moja pekee, wakati msimu uliopita alicheza mechi 34 na kufunga mabao matatu.

 

Katika msimu wa 2017/18, alifunga mabao matano katika mechi 44, msimu mmoja nyuma alicheza mechi 47 na kufunga mabao matatu.

Heshima aliyoiweka msimu wa 2016/17 na 2017/18 kwa kutoa jumla ya asisti 24, hivi sasa imeshuka kabisa. Hivyo ana kazi ya ziada.

 

KUVUNJA REKODI YA MATAJI

Paco Gento anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji wa Real Madrid aliyetwaa mataji mengi na klabu hiyo ambayo ni 23.

Anafuatiwa na Sergio Ramos, Manolo Sanchis na Marcelo, ambao kila mmoja ametwaa mataji 21.

Endapo akitwaa mataji matatu zaidi, Marcelo ataandika jina la kuwa kinara wa mataji klabuni hapo.

 

KUITUMIKIA BRAZIL

Marcelo hajaonekana kwenye kikosi cha Brazil kilichoshiriki michuano ya Copa America 2019 ambayo wenyeji Brazil walikuwa mabingwa.

Nyota huyo kwa sasa anatamani kuona anarudi kwenye kiwango chake kama zamani na kuiwakilisha Brazil katika michuano mbalimbali.

Hawezi moja kwa moja kurudi kikosini kama hajaanza kupata nafasi ndani ya Madrid, hivyo Marcelo ana kazi kubwa ya kufanya.

MADRID, Hispania

Leave a Comment