
Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Hassan Abbas, leo Mei 31, 2020 ametangaza kwamba, Serikali imeandaa mwongozo maalum wa jinsi michezo mbalimbali nchini itakavyoendelea kuanzia kesho.
Akizungumza na vyombo vya habari leo, Dk. Abbas alifafanua mambo mbalimbali kuhusu kurejea kwa michezo.
“Kama mnavyofahamu mheshimiwa Rais hivi karibuni aliruhusu michezo kuendelea kuanzia kesho, Juni 1, 2020, ligi zote zirejee baada ya kusimamishwa kwa sababu ya maambukizi ya Corona!
“Tangu Serikali ilipoazimia kwamba michezo iendelee, kumekuwa na maswali mengi kuhusu michezo itakavyoendelea.
“Tumeandaa mwongozo maalum ambao utaelekeza kila kitu. Tayari tumeusambaza mwongozo huo uliotolewa na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo pamoja na Wizara ya Afya. “Maelekezo ya kwanza ni kwamba wadau wote wa michezo wanatakiwa kusoma mwongozo maalum uliotolewa na kuutekeleza,” alisema Dk. Abbas na kuongeza.
”Serikali imeridhia mashabiki watakaotaka kwenda uwanjani wahudhurie mechi kama ilivyokuwa awali lakini wazingatie kukaa mita moja wakati wa kuingia na kuangalia mechi uwanjani, kuvaa barakoa pomoja na viwanja kuwekewa maji tiririka ili wanawe,”alisema Dk. Abbas.
Aidha, alisema kwa mechi kubwa ambazo zinaweza zikasababisha uwanja kujaa na ile kanuni ya mashabiki kukaa mita moja isizingatiwe, Serikali imeagiza utaratibu wa kuingia mashabiki nusu ya uwezo wa uwanja husika ili kuendelea kuchukua tahadhari.
Kwa upande wake Rais wa TFF, Wallace Karia alisema;
“Sisi kama TFF tunaishukuru Serikali kwa kuruhusu michezo kurejea na tutazingatia kanuni za usalama wa afya ambazo zimetolewa na niwaombe wadau wakiwemo mashabiki wazingatie sana.”