×

Maalim Seif Atoa Mapendekezo ya Uchaguzi wa Haki, Huru…

MWENYEKITI  wa chama cha  ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad,  leo Juni 10, 2020, ametoa mapendekezo kumi ya chama chake kwa wadau wa siasa ambayo yataufanya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu  nchini uwe huru, wa haki na katika mazingira ya usalama.

Ameyasema hayo akati akiongea na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho yaliyoko Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa mambo aliyotaka yafanyike kabla ya uchaguzi huo ni kuondolewa kwa sheria 40 ambazo zilizotajwa katika Tume ya Nyalali wakati wa kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Pia alitaka kuundwa kwa tume huru za uchaguzi Bara na Visiwani badala ya zile ambazo huteuliwa na marais wa sehemu hizo ambao ni makada wa Chama Cha Mapinduzi  (CCM) ambacho ndicho chama tawala nchini.

Alitaka pia kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika jana (2019) katika mazingira yasiyokuwa huru na haki, akisema waliotokea kushika nafasi hizo hawakutokana na vibali vya wapiga kura, yaani wananchi.

Alisisitiza pia kwamba vyombo vya usalama na ulinzi ambavyo ni vyombo vya dola, visiendelee kutumika kukisaidia CCM, hali ambayo alisema imekuwa ikitumika wakati wote.

Masuala mengine aliyosisitiza ni kwa vyombo vya habari kutoa fursa sawa kwa vyama vyote kufikisha ujumbe wake kwa wananchi bila ya upendeleo wowote, tofauti na sasa ambapo vyombo hivyo vinatumiwa pekee na chama tawala cha CCM.

Pia alitaka vyama vya upinzani vipewe fursa zote zinazotakiwa kikanuni, ikiwa ni pamoja na kupata daftari za wapiga kura na hati zote zinazohusika katika mchakato wa kupiga kura, kuhesabu na kutangazwa kwa matokeo ya mwisho.

Alionya kwamba kuna dalili zinaoonyesha kwamba hali hiyo itabaki kama ilivyo, jambo ambalo alisema linaweza kuingiza nchi katika mazingira mabaya.

“Kwa msingi huo, ACT Wazalendo tunawasilisha hoja kwa wadau wa uchaguzi kuhusu mapungufu yaliyopo na mapendekezo yetu kuhusu masharti ya lazima kwa uchaguzi kuwa huru,” alisema.

 

Leave a Comment