
“Kila nilipokuwa nikitaka kung’atuka walikuwa wakiniambia; ‘Mwalimu endelea tu, hii ni nchi changa na umeitoa mbali. Nchi hii haitaendelea bila wewe’. Nami niliendelea hadi pale nilipokuja kugundua kumbe nchi changa wanayoiongelea ni familia zao, hazitaendelea bila mimi kuwepo madarakani, maana walikuwa hawana uhakika kama Rais ajaye atawaacha katika nafasi walizokuwa nazo”. Hayo ni maneno katika moja ya hotuba za Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Nukuu hii imeendelea kuishi hadi sasa, imelandana na kile kinachoendelea miongoni mwa wanaCCM ambao wanapigia chapuo kila mara kumtaka Rais John Magufuli aendelee hata pale muda wa ukomo wake wa urais utakapokamilika kwa mujibu wa Katiba mwaka 2025.
Rais Magufuli ambaye anatarajiwa kutetea kiti hicho mwaka huu kwa mujibu wa Katiba, ni moja ya marais waliokosha nyoyo za Watanzania waliowengi kutokana na kasi, uweledi na umakini wa kutekelezaji majukumu na kuisimamia serikali.
Hata hivyo, kabla ya kuutetea muhula wa pili, tayari kumekuwapo na mapambio kutoka kwa makada wa CCM ambao wanamtaka kiongozi huyo abadilishe Katiba ili imruhusu kugombea tena muhula wa tatu.
Kauli ya hivi karibuni ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kwamba Rais Magufuli atake asitake ataongeza muda, ndio kauli iliyozidisha mjadala kuhusu suala hilo.
Ikumbukuwe kuwa kauli hiyo ya Ndugai ilitokana na azimio la Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy (CCM) la kuomba Bunge kumwongezea muda Rais Magufuli mara baada ya kumaliza kipindi chake cha pili cha uongozi mwaka 2025.
“Labda nyinyi hamsumbuliwi, mimi nasumbuliwa, kuna nchi zingine wanapingwa na wameuawa kwa ajili ya Corona. Katiba sio msahafu, inabadilishwa wakati wowote na anakuwa sio Rais wa kwanza, alazimishwe atake asitake, haiwezekani kumwachia nafasi, nataka alazimishwe tu,” alisema Kessy.
Aidha, Spika Ndugai alichagiza kuwa; “Mheshimiwa ngoja twende kwenye Uchaguzi Mkuu turudi, naamini wote tunarudi, hilo lishike uwe nalo na azimio litapita kwa kishindo atake asitake ataongeza muda (Rais Magufuli.
“Nikuhakikishie Bunge hili ndiyo lina mamlaka ya kutengua hilo, yeye amekuwa nani asiombwe, lazima aongezewe muda atake asitake.”
Ikumbukwe kuwa kauli hiyo ya Ndugai na Kessy, si viongozi wa kwanza kupendekeza matamanio hayo, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda Disemba 19 mwaka jana alisema “Mimi napata matumaini sana, miaka hii 10 uliyopewa itatupeleka pazuri sana. Ni kwa kuwa tu Katiba zenyewe ziko tight (zimebana), lakini kama si kwa sababu hiyo, Wallah ningezema mzee ungeongeza tena, piga kama mitano tu”.
Lakini pia Hoja ya kuongeza ukomo wa urais ilianza kuibuliwa Septemba 12, 2017 Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), aliwasilisha kusudio lake la muswada binafsi wa mabadiliko ya Katiba unaohusu kuongeza ukomo wa ubunge ambao ndani yake kuna hoja ya ukomo wa madaraka ya urais kuwa miaka saba, badala ya mitano.
Hata hivyo, katika kile ambacho Rais Magufuli anaamini kuwa si jambo la kiungwana, mara kadhaa amekuwa akisisitiza kutoongeza muhula wa tatu pindi atakapofanikiwa kunyaku muhula wa pili.
Kila mara amekuwa akieleza namna majukumu ya urais yanavyochosha lakini pia akasisitiza kumweka Mungu mbele katika suala hilo.
“Sijabadilika naomba Mungu asinibadilishe, niendelee kumtegemea Mungu. Mimi ni Magufuli yuleyule niliyekuwa ninapita hapa nauza maziwa…, kazi hizi ni za kupita na maisha yetu ni ya kupita.
“Kwa kuzingatia sheria na Katiba sitegemei kuongeza hata siku moja nikishamaliza muda wangu, narudia tena sitegemei kuongeza hata siku moja baada ya kumaliza muda wangu. Kwa sababu muda nitakaokuwa nimepewa kwa mujibu wa Katiba ndio nitakaokuwa nimepewa na Mungu kuwatumikia Watanzania,” Rais Magufuli alitoa kauli hii mwaka jana.
Licha ya maneno ya hisia na msisitizo namna hii, sasa Bunge linaelekea kuamua kumlazimisha kuendelea muhula wa tatu, licha ya kwamba muhula wa pili bado hajautetea na kuumaliza.
Hali hii inashangaza na kuibua maswali kadhaa hususani kwa waimba mapambio ya aina hii.
Kwamba makada hawa ni makada waandamizi ndani ya CCM, si makada walioubuliwa ndani ya CCM kipindi cha uongozi wa Magufuli, kwa sababu baadhi yao walikuwepo uongozi tangu utawala wa Mwalimu Nyerere, Mkapa na Kikwete. Cha ajabu sasa ndio wamemuona Magufuli ndiye mtu pekee anayepaswa kuivunja Katiba jambo ambalo kidogo linafikirisha kwamba je, wanamtakia mema au mabaya dhidi ya maamuzi hayo.
Ni kweli usiopingika kuwa hakuna Rais aliyefanya mambo yanayoonekana kukosha nyoyo za Watanzania kama ilivyo kwa Rais Magufuli, kwa sababu, kuanzia miundombinu, usafirishaji, rasilimali na ahadi kemkem amejitahidi kuzitekeleza licha ya baadhi ya watanzania kunung’unika ukata kimaisha.
Kwa mantiki hiyo, maamuzi wanayopendekeza viongozi hawa kumlazimisha aongeze muhula wa tatu, aidha wanataka kuzusha yale yaliyotokea Burundi mwaka 2015 baada ya Pierre Nkurunziza kuibadilisha Katiba na kujiongezea muda au wanataka kushibisha familia zao changa kama Mwalimu Nyerere alivyosema.
Nasema hivyo kwa sababu ni dhahiri huwezi kutafsiri moja kwa moja dhamira ya mtu kwa kile anachokizungumza, kwamba ndani ya moyo wake amelenga nini kitokee, au afaidikike na kipi.
Kwa maana hiyo, ni vema kuuishi ule msemo aliyotuachia Rais mstaafu Jakaya Kikwete kwamba akili za kuambiwa changanya na zako.
NA GABRIEL MUSHI