
MERCY Mukandara, mkazi wa Kimara Stop Over jijini Dar es Salaam, ameuawa na mumewe Erick Samson Kuberwa au la; ni kazi ya vyombo vya dola kutoa jibu la swali hilo, IJUMAA WIKIENDA limesheheni ripoti kamili chini ya kapeti Juni 16, mwaka huu, Mercy alifariki dunia kwa kile alichodai mumewe kuwa ni kujigonga kwenye meza baada ya kupigwa na shoti ya umeme, jambo ambalo ndugu wa marehemu wamesema “Hapana” na tuhuma nzito kumwangushia Erick ambaye anashikiliwa na polisi kwa sasa kuwa ndiye aliyemuua.
MASHUHUDA
Kwa mujibu wa mashuhuda, mwili wa marehemu ulikutwa na jeraha kichwani huku kitanda alichokuwa amelala na mumewe, kikiwa kimelowa damu.
Polisi kupitia kamanda wake wa mkoa wa Kinondoni Edward Bukombe, wamesema wanafanyia uchunguzi mzito tukio hilo.Bila shaka uchunguzi huo utajikita katika kuangalia chanzo cha shoti ya umeme, marehemu alipigwaje na shoti hiyo usiku wa manane na mambo mengine ambayo yamewatia mashaka ndugu na marafiki wa marehemu.
WIKIENDA NA RIPOTI KAMILI
Ingawa polisi ndiyo wenye jukumu la kuja na ripoti ya kifo, IJUMAA WIKIENDA lilijikita katika kuchunguza mambo ya chini ya kapeti yaliyokuwepo kati ya marehemu na mumewe.
Rafiki wa karibu na marehemu ambaye aliomba jina lake lifichwe aliyedai pia kusoma na Mercy Shule ya Sekondari Tusiime mwaka 2003, aliiambia timu yetu ya uchunguzi kuwa:
“Nimesoma na marehemu shule moja, nilikuwa mtu wake wa karibu na mshauri wake pia.“Nakumbuka aliwahi kuniambia kuwa hakuwa na furaha na ndoa yake kwa sababu mumewe alikuwa akimsema vibaya kuwa hana uzazi.“Kutokana na sababu hiyo, Mercy aliniambia kuwa mume wake amebadilika kitabia na kwamba anajihusisha kimapenzi na wanawake wengine na alipogundua na kumuuliza, alimjibu kuwa anatembea na wanawake wengine kwa ajili ya kutafuta mtoto.
”CHUKI KWA MTOTO WA MAREHEMU
Chanzo kingine kililiambia WIKIENDA kuwa, marehemu Mercy alikuwa akilalamika kuwa mumewe hakuwa na mapenzi na mtoto wake wa miaka mitano aliyezaa na mwanaume mwingine.“Marehemu aliniambia hata wiki haijaisha kuwa alikuwa na hofu kuwa huwenda mume wake angekuja kumdhuru mtoto, hivyo alikuwa amepanga waachane lakini mwanaume akawa hataki,” kilisema chanzo chetu.Kiliongeza kuwa, mara ya mwisho ugomvi kati ya wanandoa hao ulitokea siku tatu kabla ya tukio, hoja ikiwa ni nani aondoke kwenye nyumba mume au mke.
“Inadaiwa mume alimwambia mwanamke kuwa aondoke arudi kwao Mwanza lakini mke akasema hawezi kuondoka kwa sababu kodi ya nyumba analipa yeye, kama wa kuondoka aondoke mwanaume ambaye naye alikataa,” chanzo kilisema.Hata hivyo, haijafahamika nyuma ya mgogoro huo kimetokea kitu gani ambacho ndugu wanakiona kama sababu ya kumtuhumu mumewe kuhusika na kifo cha Mercy.
MVUTANO WA MAZISHIAkizungumza na WIKIENDA, mama mkubwa wa marehemu, Letisia Katunzia alisema:“Nimeumizwa na kifo cha mwanangu, miaka miwili tu kwenye ndoa anakufa katika mazingira yenye utata.“Lakini kwa kuwa imetokea hivyo, basi tulikutana na baadhi ya ndugu wa mwanaume, ikaonekana kwamba tuhamishie msiba kwa mjomba wa mwanaume.“Sisi tumekataa, tumewaambia kuwa tutabaki hapahapa kwa sababu marehemu ndipo alipokuwa akiishi.
“Ndugu wa mwanaume wakaondoka, baada ya muda wakarudi na kusema wamefanya kikao wao kama wao na wameamua msiba uwe kwao.
“Tukawaambia sisi hatuwezi kuondoka hapa kwa sababu kwanza mlango umefungwa kwa ajili ya usalama.“Kingine marehemu alisema kuwa akifariki anaomba asizikwe upande wa ukweni kwake na badala yake azikwe kwa baba yake.“Aliongea hivyo kwa sababu kulikuwa na migogoro mingi baina yake na mumewe, hivyo hata maisha yake ya ndoa ni kama alikuwa anaishi kwa kuvumilia tu,” alisema Letisia.Hata hivyo, baadaye mwafaka ulifikiwa baina yao hivyo mwili wa marehemu kukabidhiwa kwa ndugu zake ambapo jana (Jumapili) ulitarajiwa kuagwa na kusafirishwa kwenda Bukoba kwa mazishi.
DADA WA KAZI NAYE AZUA NENO
Wakati hayo yakiendelea, mama mdogo wa marehemu, Doris Fredrick alisema walitegemea kumkuta dada wa kazi ambaye alikuwa akiishi na marehemu, lakini cha kushangaza ni kwamba, ndugu wa mwanaume waliwahi kumchukua na kumficha.“Huyu alikuwepo siku ya tukio na anajua mengi, lakini tumekuja hapa ndugu wa mwanaume wameondoka naye.“Hebu jaribu kujiuliza sisi ndugu wa marehemu hata kabla hatujafika hapa msibani, wenyewe tayari wamemchukua dada wa kazi kwa sababu gani?“Marehemu alikuwa na mtoto wake anayeishi naye hapa na yule mfanyakazi yupo kwa ajili ya yule mtoto, lakini mtoto wa marehemu ambaye ni mdogo wamemuacha, wao wameondoka na mtu wa kumtunza na wanajua fika mama yake mzazi amefariki.“Tulipouliza binti wa kazi yupo wapi wakasema watamsafirisha kwa ndege ili aende kwao, lakini siyo kweli wanamficha yule binti kwa sababu wanahisi ana ushahidi wa kutosha, yule binti sisi ndiyo ambao tulimtafuta hivyo tunajua wapi anatokea na familia yake ipo wapi.“Sasa wao anawahusu nini, wangekuwa ni watu wema wangemjali zaidi mtoto wa marehemu kuliko dada wa kazi ambaye hawamjui kwa lolote,” alisema Doris.
MTUHUMIWA NA SHULE YA UPADRI
Aidha, WIKIENDA lilidokezwa kuwa mume wa marehemu Mercy, Erick ni kijana ambaye amekulia katika maadili ya dini ya Kikristo hasa imani ya Kanisa Katoliki.“Mimi namfahamu vizuri Erick, amewahi kusomea upadri hadi kwenye hatua za mwisho lakini haijulikani kilitokea nini akaachishwa.“Lakini ndoto yake kubwa katika maisha yake ilikuwa ni kumtumikia Mungu, nakumbuka aliwahi kutumikia kanisa Katoliki Parokia ya Kwa Mathias, Kibaha mkoani Pwani.“Aliacha masomo ya upadri hakurudi kwao Bukoba, ndiyo wakakutana na huyu Mercy miaka miwili iliyopita wakaoana.“Najua mengi yaliyokuwa yakiendelea kwenye ndoa yao, lakini kwa kuwa mmoja hayupo, si vyema kuzungumza, utakuwa unaongelea upande mmoja,” alisema kijana mmoja ambaye alidai kuwa ni mtu wa karibu na Erick.
UJUMBE KWENYE DIARY WAZUA UTATA
Katika hatua nyingine, chanzo kingine kililiambia WIKIENDA kuwa ndani ya kitabu cha kumbukumbu cha Erick walikuta ujumbe mwingi huku mmoja ukizua utata.“Inaonekana (Erick) anatabia ya kuandika vitu vyake kwenye diary yake na ujumbe wa mwisho aliandika, ‘sijutii kwa hiki ninachokifanya.’“Sasa sijui ndiyo hii tuhuma ya mauaji au kuna jambo jingine alimaanisha kuwa atalifanya na hatajutia,” chanzo kilisema.Hadi tunakwenda mitamboni, mvutano wa mazishi ulikuwa unaendelea na kwamba mtuhumiwa alikuwa akishikiliwa na jeshi la polisi huku ndugu wa marehemu Mercy wakisubiri kwa hamu ripoti ya kifo chake.Timu ya Global Publishers inaendelea kufuatilia kwa undani tukio hilo, hivyo endelea kufuatilia kupitia Magazeti Pendwa, Global TV Online, +255Global Radio na mitandao yetu mingine ya kijamii
⚫️ Kwa UPDATES zote, Download GLOBAL APP: ⚫️ ANDROID:http://bit.ly/38Lluc8 ⚫️ iOS:https://apple.co/38HjiCx