×

Wawa Kucheza Fainali Dhidi Ya Namungo FC

BEKI wa kati wa Simba, Muivory Coast, Pascal Wawa, anatarajiwa kuwepo kwenye sehemu ya kikosi kitakachoivaa Namungo FC katika mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho, maarufu kama FA.

 

Muivory Coast huyo, Alhamisi alipewa kadi mbili za njano kabla ya kupewa nyekundu na kutolewa nje katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

 

Fainali ya FA inayotarajiwa kujaa upinzani mkubwa, imepangwa kupigwa Agosti 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, Ruangwa.

 

Kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu Bara, kifungu cha 38 kifungu kidogo cha kwanza: “Mchezaji atakayetolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kadi mbili za njano (second yellow card) katika mchezo wa ligi, hataruhusiwa kucheza mchezo mmoja unaofuata wa timu yake.”

 

Hivyo, mchezo uliofuata wa Simba ulikuwa jana Jumapili dhidi ya Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi na beki huyo hakucheza mchezo ule.

 

Wawa anatarajiwa kuwa huru katika mchezo unaofuata wa fainali hiyo ya FA kama Kocha Mkuu wa timu hiyo Mbelgiji, Sven Vandenbroeck, akihitaji kumtumia watakapocheza dhidi ya Namungo.

 

Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, alithibitisha hilo kwa kusema: “Kanuni zipo wazi, Wawa atakuwepo sehemu ya kikosi chetu kitakapocheza fainali ya FA, ni baada ya kumaliza adhabu yake ya kadi nyekundu tulipocheza na Coastal.”

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave a Comment