×

Mwalimu Aacha Kazi, Awa Hausigeli

MACRINE OTIENO, aliyekuwa mwalimu katika shule ya msingi binafsi ya Chrives Royal jijini Nairobi, sasa amelazimika kufanya kazi ya ujakazi ili kujikimu kimaisha katika mazingira ya sasa ya maambukizi ya virusi vya corona.

 

Macrine ni mmoja wa maelfu ya walimu ambao wameathirika  zaidi kutokana na kufungwa kwa shule ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona tangu mwezi Machi mwaka huu.

 

“Wakati shule zilipofungwa, mshahara ulisimamishwa kwa kuwa nilikuwa mwalimu kwenye shule ya binafsi,” anasema Macrine.

 

Watu husema kwamba akiba haiozi, lakini akiba alizowekeza Macrine zilimsaidia kwa muda mchache kabla ya mtoto wake kuugua na kumlazimisha kutumia akiba hiyo kumtibu.

 

“Mtoto wangu aliugua kwa muda wa wiki tatu na kadi yangu ya bima ya matibabu nikawa nimeipoteza. Fedha zote nilizokuwa nazo kwenye akiba, nililazimika kuzitumia kumtibu mwanangu. Fedha zilizosalia nikatumia kulipia kodi ya nyumba,” anasema.

 

Hata hivyo, siku zilivyozidi kusonga mbele ndivyo maisha yalivyoendelea kuwa magumu kwake Macrine na mtoto wake. Chakula kikawa vigumu kukipata ikiwa ni pamoja na kulipia kodi ya nyumba.

 

“Nilianza kupokea ujumbe kutoka kwa mwenye nyumba, kwamba anataka kodi. Huku chakula hata sikuwa nacho, hata cha kumlisha mtoto pekee. Baada ya siku chache, nikafungiwa nyumba…    Nikawaza nitafute kazi ambayo itaniwezesha hata kupata fedha kidogo ambazo zingetuwezesha kuishi,” anaendelea kusimulia.

 

Mwalimu huyu ambaye amekuwa akifundisha kwa muda wa miaka sita aliamua kutafuta kazi kama kijakazi kwa msingi kwamba kazi hiyo ingempa malazi na hata chakula. Akamwomba rafiki yake amsaidie kumlea mtoto wake ili aweze kutafuta kazi hiyo ya ujakazi.

 

“Nilimchukua mtoto wangu nikampeleka kwa rafiki yangu… Nilihisi kusikitika sana kwani sijawahi  kutengana na mwanangu tangu alipozaliwa. Lakini sikuwa na budi kwa sababu nilifikiria maisha ya mtoto wangu, jinsi kwa siku kadhaa tulivyokosa hata chakula. Na nikaamua kwamba nitafanya kazi yotote ilimradi nipate mapato yatakayoniwezesha kuanzisha biashara,” anasimulia Macrine huku akilia.

 

Ninachokosa ni uhuru

Macrine aliweza kupata ajira. Baada ya siku chache akiwa kwenye kazi yake mpya, alipokea simu kutoka kwa rafiki yake kwamba aende akamchukue mwanaye. Hili lilimfanya kuvunjika moyo  zaidi kwa kuwa kazini, mwajiri wake asingemruhusu yeye kuishi na mwanaye.

Hivyo akalazimika kumpeleka kwa binamu yake. Hata hivyo haikuchukua muda, Rais Uhuru Kenyatta akafungua mipaka ya kaunti iliyofungwa kwa ajili ya kudhibiti maaambukizi ya ugonjwa wa Corona. Macrine akamtuma binamu yake kumpeleka mtoto kwa wazazi wake kwa sababu hangeweza kupewa ruhusa tena kazini.

 

“Ninachokikosa sana kwenye kazi hii ni uhuru… Ilikuwa ni vigumu sana Mimi kupata ruhusa ya kuenda kumchukua mwanangu, rafiki yangu aliponiita. Na wakati mipaka ilipofunguliwa, nilinyimwa ruhusa ya kumpeleka mwanangu kwa wazazi wangu. Kila unapotaka kufanya chochote, lazima uombe ruhusa, na ukinyimwa basi ndiyo hivyo… Huwezi kufanya lolote,” anaendelea.

 

Kila Macrine alipoziba ufa mmoja, ili asijenge ukuta, ufa  mwingine ulijitokeza. Mmiliki wa nyumba aliyokuwa akiishi Macrine, alivitupa nje vifaa vyake  kwa kuwa alishindwa kulipa kodi ya nyumba. Na kwa kuwa ilikuwa vigumu kwake kupata ruhusa kazini, ilimbidi kuwapatia jirani zake vifaa hivyo.

 

“Nilipigiwa simu na jirani yangu akaniambia kwamba mwenye nyumba amevitoa vitu vyangu nje ya nyumba na nyumba imepewa mpangaji mwingine. Nilimwaambia anisaidie kuniwekea kile ambacho angeweza kukiweka, na vingine wagawane na jirani wengine wavitumie,” anasema kwa majonzi.

 

“Ninachokikosa sana ni uhuru…” ni maneno anayoisema Macrine.

 

Katika maisha inabidi ujipange

Susan Manyala anayesimamia usajili katika kampuni ya kuwasajili vijakazi ya Nyarai Home of Humility, ambayo pia ni kampuni iliyomsajili Macrine anasema kwamba walipokea walimu wanne mwezi wa sita.

 

” Tumewasajili walimu wanne. Watatu kati yao wameshapata ajira ila mmoja aliyesalia, imekuwa ni vigumu kwake kuajiriwa kwa madai kuwa ana umri mkubwa. Ana umri wa miaka 45, na wateja wengi wanashuku iwapo ataweza kufanya kazi za nyumba,” anasema.

“Wateja wanawafurahia sana kwa sababu wanasema kwamba licha ya wao kufanya kazi za nyumbani wanaweza pia kuwafundisha watoto wao,” anasema.

 

Kazi ya ujakazi haijawa rahisi kwake Macrine, na ni matumaini yake kwamba mambo yatakuwa sawa, na hali itarejea kama ilivyokuwa awali.

 

“Inaniuma sana ila sina budi. Licha ya uchungu niaohisi, najua ni lazima nivumilie. Na nijajua ya kwamba nikitoka hapa tutakuwa pamoja na mtoto wangu. Ila nahisi kwamba siwezi kuendelea. Nasubiri fedha nitakazopata mwisho wa mwezi huu, ingawa kidogo nitaenda kuanzisha biashara…

 

“Katika maisha unapaswa uwe tayari ujipange na ujue maisha hubadilika, leo inaweza kuwa sawa kesho ikawa hali tofauti, lakini kwa chochote kile ambacho kitatokea, ni vizuri tukubali na tutafute mbinu ya kujisaidia,” anafafanua.

 

Mapema mwezi huu, Wizara ya Elimu nchini Kenya ilitangaza kwamba shule zote za msingi na za upili (sekondari) zitafunguliwa Januari mwaka  2021, hatua ambayo walielezea wamechukua ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona, hasa kwa watoto.

 

Siku mbili baada ya kufanya mahojiano haya na Macrine, alitupatia ujumbe kwamba ameiacha kazi hiyo na sasa anajiandaa kuanzisha biashara yake kwa fedha alizopata.

Leave a Comment