×

Yanga Yasajili Mashine Nne kwa Mpigo

JEURI ya fedha! Ndivyo utakavyoweza kusema hivi sasa baada ya Kampuni ya GSM kutumia Sh milioni 210 kufanikisha usajili wa wachezaji watatu mfululizo ndani ya saa 48, huku mwingine akifi chwa hotelini jijini Mwanza kuwakwepa Simba waliokuwa wakimnyatia, kabla ya kusaini miaka miwili Jangwani.

 

Katika usajili huo, mchezaji mmoja, beki Bakari Mwamnyeto, amesaini mkataba Yanga wakiwazidi ujanja Simba ambao saa chache baada ya kusaini Yanga wakiwa hawajui chochote, walimuwekea ofa ya Sh milioni 180.

 

GSM inafanya usajili huo kwa kushirikiana na Kamati ya Usajili ya timu hiyo katika kukiimarisha kikosi chao ili msimu ujao wawe tishio na kuwapoka ubingwa watani wao, Simba.

 

Yanga ndani ya siku mbili, juzi Ijumaa na Jumamosi walikamilisha usajili wa wachezaji watatu ambao ni kiungo mkabaji wa Kagera Sugar, Zawadi Mauya, beki wa kati wa Coastal Union, Bakari Mwamnyeto na beki wa kushoto wa Polisi Tanzania, Yassin Mustapha ‘rasta’.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, kwa wachezaji hao watatu wametumia gharama ya Sh milioni 210 kufanikisha usajili wa nyota hao.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa katika hizo Sh mil 210, Mwamnyeto amechukua Sh mil 150 zilizomshawishi staa huyo wa Coastal kumwaga wino Jangwani. Lakini muda mchache baadaye, alipokea simu ya ofa ya Simba ya Sh mil 180 lakini tayari ilikuwa ‘too late’ kwa kuwa alikuwa ameshamwaga wino Jangwani.

 

Aliongeza kuwa, Mustapha na Mauya kila mmoja amechukua Sh mil 30 na kufi kia Sh 60Mil ambazo ukizijumlisha na za Mwamnyeto, zinafi kia jumla ya 210 Mil.

 

“Bado uongozi wa Yanga kwa kushirikina na GSM unaendelea na usajili wao, walianza na usajili wa wachezaji wazawa ambao umekamilika kwa asilimia mia moja, bado wachezaji kama wawili ili kukamilisha usajili wa wazawa.

 

“Kwani tayari tumekamilisha usajili wa Mauya, Mustapha na Mwamnyeto ambao wote ni wazawa baada ya kumalizana na hao tunaelekeza nguvu kwa kiungo mshambuliaji mmoja mzawa ambao ndani ya siku hizi mbili utakuwa umekamilika.

 

“Baada ya hapo nguvu tunazielekeza kwa wachezaji wa kimataifa ambao kuanzia leo (jana) wataanza kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) tayari kwa ajili ya vipimo vya afya na kusaini mikataba.

 

“Wachezaji wanaotarajiwa kutua siyo majina mageni mdomoni mwa watu kutokana na kati yao kutajwa kwenye Vyombo vya Habari kuwa watajiunga na Yanga kwenye msimu ujao,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said, kuzungumzia hilo, alisema: “Mkataba ni siri ya mwajiri na mwajiriwa, hivyo ni ngumu kutaja dau la usajili la mchezaji.

 

“Hivi sasa uongozi upo kwenye mipango ya kukisuka kikosi kitakachokuwa imara na tishio kitakachokuwa bingwa kwenye msimu ujao, tayari tumemalizana na Mwamnyeto, Mustapha na Mauya waliokuwa kwenye mipango yetu.”

 

Yanga pia muda wowote kuanzia jana walitarajia kumtangaza mtambo wa mabao, Waziri Junior kutoka Mbao FC ambaye inaelezwa ameshasaini mkataba wa miaka miwili.

 

Waziri ndiye kinara wa mabao kwenye Klabu ya Mbao akifunga jumla ya mabao 14 katika mashindano yote na kutoa asisti nne. Waziri amefunga mabao 12 kwenye Ligi Kuu Bara na mawili kwenye mashindano ya FA, licha ya timu yake kushuka daraja.

 

Taarifa kutoka kwenye kambi ya Mbao FC zinasema kuwa mchezaji huyo alitarajiwa kupandishwa ndege na mabosi wa Yanga juzi Jumamosi mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Play Off dhidi ya Ihefu ulioshuhudiwa Mbao akishushwa daraja kwa kanuni ya mabao ya ugenini licha ya kushinda 4-2, kwa sababu walifungwa 2-0 katika mchezo wa kwanza.

 

Lakini ndege ya usiku ilikosekana, hivyo akachukuliwa kuhifadhiwa hotelini na mmoja wa matajiri wa Mwanza ambaye ni Yanga lialia aitwaye Yanga Makaga.

 

“Baada ya kufi chwa, haraka mwanasheria wetu, ambaye ni kaimu katibu mkuu wetu (Patrick Simon), leo (jana) aliondoka na ndege ya alfajiri kwa ajili ya kumalizana naye ambaye tumefi kia muafaka na usiku wa leo (jana) atakuwa amesaini mkataba,” alisema mtoa taarifa kutoka Mwanza.

 

Alipotafutwa Waziri ili azungumzie suala hilo la Yanga alisema: “Kwa sasa naenda kwanza nyumbani kupumzika, kisha baada ya hapo ndiyo nitajua, ukweli ni kwamba nina ofa nyingi sana mezani, hivyo tuendelee kusubiri muda ufi ke.”

 

Kwa upande wa Yanga alitafutwa Ofisa Mhamasishaji wa klabu hiyo, Antonio Nugaz ambaye alisema: “Kiukweli Yanga imedhamiria kufanya maboresho ya kikosi chake, na ni kweli leo (jana) Jumapili tutamtangaza mchezaji lakini siwezi kukuambia ni mchezaji gani, endelea kuvuta subira ndugu yangu.”

 

Hadi sasa Yanga imesajili wachezaji wawili kwenye safu ya ulinzi kwa maana ya beki wa kushoto ni, Yassin Mustapha aliyetoka Polisi Tanzania, beki wa kati ni, Bakari Nondo Mwamnyeto aliyetoka Coastal Union na kiungo Zawadi Mauya aliyetokea Kagera Sugar.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave a Comment