×

Mlipuko Waua 78, Waharibu Majengo Beirut – (Video +Picha)

LEBANON inaomboleza baada ya mlipuko mkubwa katika mji mkuu wa Beirut kuwaua watu 78 na kuwajeruhi wengine 4000 jana  (Jumanne).

Mji wote uliyumbishwa na mlipuko huo, ulioanza kwa moto katika bandari kabla mlipuko huo uliofanana na wingu la uyoga kutokea.

Rais Michel Aoun alisema kwamba tani 2,750 za ammonium nitrate zilikuwa zimewekwa vibaya katika ghala moja kwa miaka sita.

Aliitisha kikao cha dharura siku ya Jumatano  na kusema hali ya dharura ya wiki mbili imetangazwa.

Aoun pia alitangaza kwamba serikali itatoa Dola mil. 66 za hazina ya dharura.

 

”Kile tunachoshuhudia ni janga kubwa’,’  alisema mkuu wa kundi la Msalaba Mwekundu, George Kettani, akizungumza na vyombo vya habari na kuongeza:  ”Kuna waathiriwa kila mahali”.

Maafisa walisema siku ya Jumanne kwamba uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo kilichosababisha mlipuko huo.

Baraza kuu la ulinzi nchini Lebanon lilisema kuwa wale waliohusika wataadhibiwa vilivyo.

Ammonium Nitrate ilikuwa imeshushwa kutoka katika meli iliyokamatwa katika bandari hiyo 2013 na kuwekwa katika ghala.

Mlipuko huo unajiri wakati mgumu kwa upande wa taifa hilo, huku likikabiliwa na mgogoro wa kiuchumi unaosababishwa na mgawanyiko wa jadi na taifa hilo likiathiriwa na mgogoro mwengine wa virusi vya corona.

Hali ya wasiwasi pia iko juu kabla ya uamuzi wa siku ya Ijumaa kuhusu kesi ya mauaji ya aliyekuwa Waziri Mkuu,  Rafik Hariri 2005.

    

 

Leave a Comment