
MAKAMU wa Rais wa Zimbabwe, Constantino Chiwenga, amechaguliwa kuwa Waziri wa Afya, mwezi mmoja baada ya kuibuka kwa kashfa dhidi ya vipimo vya corona na vifaa vya afya.
Jenerali Chimwenga ni mkuu wa zamani wa jeshi aliyeongoza mapinduzi ya kumuondoa madarakani rais wa zamani wa nchini humo, Robert Mugabe.
Aliyekuwa waziri wa afya, Obadiah Moyo, alifikishwa mahakamani mwezi Juni kujibu mashtaka ya rushwa ya Fola milioni 20 ambayo anadaiwa kupokea wakati wa kuingia mkataba na kampuni moja kutoka nchini Hungary.
Moyo alidaiwa kutofuata utaratibu sahihi, na sasa yupo nje kwa dhamana.
“Rais Mnangagwa alieleza kuhusu uharaka unaohitajika ili kubadili mfumo wa afya hasa katika kukabiliana na janga la corona,” taarifa kutoka ofisi ya rais imesema.
Zimbabwe imethibitisha kuwa na visa vya corona 4,200, vikiwemo vifo 81 vilivyotokana na maambukizi hayo ingawa inadaiwa kuwa maamnukizi ni makubwa zaidi.