×

Polepole: Chadema Nawaachia Watanzania – Video

KATIBU wa Itikadi na Uenezi (CCM), Humphrey Polepole,   wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ameeleza kusikitishwa kwake na kitendo cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kubadili maneno ya moja ya ubeti wa Wimbo wa Taifa wa Tanzania na kuweka maneno ya Chadema wakati wakiimba kwenye moja ya vikao vyao juzi.

 

Polepole amesema hayo leo Jumatano, Agosti 5, 2020 wakati akizungumza na vyombo vya habari katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM (OND) Lumumba Jijini Dar es Salaam. 

 

“Mimi hiki chama nimeshindwa kukielewa, nidhamu ni zero, kutii sheria bila shuruti ni zero, siku wanampokea jamaa yao mgonjwa pale Airport, ilikuwa ni vurugu tupu, wanapita barabara zote, bila kujali wapo watakaotumia barabara hiyo kwenda hospitali na makazini.

 

“Unawaambia jamani piteni moja hawaelewi, wanapita huku mara kule, wamepita barabara zote na sio kwamba walikuwa wengi, walipofika ofisi zao pale Ufipa wakasema mbona hawajatukamata? Ina maana mpango wao walitaka wakamatwe.

“Kama haikutosha ikaja ya wimbo wa Taifa, bila aibu wanajenga hoja tuambieni wapi tunavunja sheria. Uwe Mmakonde, Msukuma, Mnyaturu, Mnyamwezi, Mkiristo au Muislam ama mshirikina, huu wimbo ni wetu sote, ukisema ‘Sala ya Baba Yetu’ hiyo haichakachuliwi, hata kama baba yako mzazi unampendaje huwezi kusema ‘Baba Yangu Mzazi aliye Mbinguni.’

“Kuna sheria hapa nchini inayosema mchukue mke wa kaka yako? Lakini ukimchukua mke wa kaka yako ni halali? Tuna katiba, sheria, kanuni, taratibu, desturi, mila na utamaduni katika kufanya mambo yetu, siyo kila jambo lazima liwe kwenye katiba lisipoandikwa ndipo utumie mwanya huo kuharibu.
“Wimbo wa Taifa ni sala, ni alama na utambulisho wetu, ni umoja wetu, mimi nawaachia Watanzania, chama ambacho kabla hujaomba ridhaa ya kuchukua nchi ushabadili wimbo wa taifa kuufanya wimbo wa chama chao, Chadema wawaombe radhi wananchi kwa kubadili maneno ya wimbo wa taifa na kuweka ya Chadema, lakini kwa ninavyowajua hawataomba radhi, kama mnabisha tubeti.
“Tatizo lingine la hawa watu wanabeza kila kitu, jamaa yao (Lissu) amekuja wamempitisha Fly-Over ya Ubungo wanajifanya hawaoni, meli ya MV. Victoria, Ndege 11, elimu bila malipo, vituo vya afya 887, Mradi wa Standard Gauge, lakini hawaoni yote chini ya Rais Magufuli, hawa jamaa hawaoni, wanatukana tu, wakati mwingine ukiwa na watu wa namna hii unapaswa kuwa mvumilivu tu wa kisiasa,” amesema Polepole.

Leave a Comment