
BAADHI ya maafisa wa mji wa Beirut nchini Lebanon wamewekwa katika kifungo cha nyumbani huku wakisubiri uchunguzi kuhusu mlipuko mkubwa wa siku ya Jumanne uliosababisha zaidi ya watu 135 kuuawa nchini humo.
Manal Abdul Samad Najd, Waziri wa Habari wa Lebanon, amesema kifungo cha nyumbani kitawashirikisha maafisa wote wa bandari ambao walihusika katika suala la kuhifadhi ‘amoniamu naitreti’ wakiilinda na kusimamia usimamizi wake tangu Juni 2014.
Wakati huo huo, Wizara ya Afya ya Lebanon imetangaza kuwa idadi ya watu waliofariki dunia katika mlipuko huo wa juzi (Jumanne) imeongezeka na kufikia wahanga 135 huku waliojeruhiwa wakiwa takriban 5,000.
Mlipuko huo ulitokea katika ghala nambari 12 la Bandari ya Beirut na kwamba sababu ya moto ni mada za milipuko ambazo zilikuwa zimehifadhiwa hapo.

Mlipuko huo ulikuwa mkubwa kiasi cha kusikika kilomita nyingi kutoka eneo la tukio. Taarifa zaidi kutoka Beirut zinasema mlipuko huo umesababisha hasara kubwa kwa nyumba za makazi na pia katika idara binafsi na za serikali hasa majengo yaliyokuwa karibu na tukio hilo.
Kwa mujibu wa Rais Michel Aoun, tani 2,750 za mada za ‘amoniamu naitreti’ zinazotumika kwa utengenezaji wa mbolea na mabomu zilikuwa zimehifadhiwa katika bandari ya Beirut kwa muda wa miaka sita bila kuchukuliwa tahadhari za kiusalama.