
SIMBA haitaki masihara rasmi sasa itasajili wachezaji sita pekee katika kukiimarisha kikosi chao kinachojiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2020/2021.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu timu hiyo iweke historia ya kubeba makombe matatu katika msimu uliopita kwa kuchukua Ngao ya Jamii, ligi na Kombe la FA.
Simba hadi hivi sasa tayari imefanikisha usajili wa mchezaji mmoja aliyesaini mkataba wa miaka miwili ambaye ni Ibrahim Ame ‘Varane’ akitokea Coastal Union ya mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, kati ya wachezaji sita, watatu ni wazawa na wengine kutoka nje ya nchi waliopo katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wao.
Mtoa taarifa huyo aliwataja wachezaji wazawa ambao tayari wameshamalizana nao kuwa ni beki wa Lipuli FC, David Kameta ‘Duchu’, mshambuliaji wa KMC Charles Ilanfya na Ibrahim Ame aliyetokea Coastal Union yeye tayari ametambulishwa baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili.

Aliwataja wachezaji kutoka nje ya nchi kuwa ni Joash Onyango anayeichezea Gor Mahia ya nchini Kenya, Mghana Bernard Morison na straika mkali wa kucheka na nyavu kutoka Lusaka Dynamo ya nchini Zambia.
Aliongeza kuwa, straika huyo Mzambia ambaye jina lake linafichwa usajili wake umependekezwa na kiungo wa timu hiyo Mzambia, Clatous Chama ambaye amewaambia mabosi wake kama wanahitaji mshambuliaji, basi wamsajili nyota huyo mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao.
“Simba tayari imekamilisha usajili wa beki mmoja pekee ambaye ni Ame kutoka Coastal, hivyo bado wachezaji wawili pekee kwa nafasi za wachezaji wazawa walizozibakisha na tayari wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wao.
“Nao ni Kameta na Ilanfya ambao wote hao muda wowote watasaini mikataba baada ya kufikia makubaliano mazuri ya kusaini, pia kwa wachezaji kutoka nje ya nchi tumepanga kusajili watatu pekee na kufikia idadi ya wachezaji sita.
“Wachezaji hao kutoka nje ya nchi yupo beki Onyango, winga Morrison na mshambuliaji Mzambia ambaye yeye usajili wake ulipendekezwa na Chama ambaye anafahamu umahiri wake mzuri wa kufunga mabao,” alisema mtoa taarifa huyo.