KIUNGO mshambuliaji wa zamani wa Coastal Union na pia msanii wa Bongo Fleva, Ally Saleh ‘Kiba’, amesema kuwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mghana, Bernard Morrison ni msaliti.
Kauli hiyo aliitoa mara baada ya mchezo wa Samakiba uliowakutanisha wachezaji wakubwa mastaa na wasanii mbalimbali uliomalizika kwa Team Kiba kuifunga Team Samatta mabao 3-1.
Katika mchezo huo mabao ya Team Kiba yalifungwa na Ibrahim Ajibu, Hassan Dilunga wanaoichezea Simba na Mudathir Yahaya anayekipiga Azam FC.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Alikiba alisema kuwa ameshangazwa na kitendo kibaya cha usaliti kilichofanywa na Morrison baada kuhama timu yake na kwenda kucheza kwa Samatta.
Alikiba alisema kiungo huyo siku zote alifanya mazoezi katika timu yake lakini akashangaa akamuona siku ya mechi akiichezea Team Samatta bila ya kumpa taarifa.
“Morrison ni msaliti, hivyo ndivyo nitakavyoweza kusema, ni baada ya kufanya mazoezi ya pamoja kwa siku zote tulizofanya, lakini baadaye nikamshangaa kumuona siku ya mechi akiichezea Team Samatta.
“Lakini hamna shida licha ya kucheza huko, lakini ameshindwa kuonyesha ubora wake ikiwemo kukosa penalti mbili huku tukiifunga hiyo timu yake aliyokwenda kuichezea,” alisema Alikiba.
CAREEN OSCAR, Dar es Salaam
