×

Morrison Aanza Kazi Rasmi Simba Kesho

KESHO Jumatatu, kikosi cha Simba kinatarajiwa kuanza mazoezi rasmi kujiandaa na msimu ujao wa 2020/21 kikiwa na nyota wake wote wapya wa zamani na wa sasa akiwemo Mghana, Bernard Morrison.

 

Wakati kikosi hicho kikianza mazoezi, Kocha Mbelgiji, Sven Vandenbroeck ambaye yupo kwao Ubelgiji, anatarajia kuwasili haraka muda wowote kuanzia sasa ili kuwahi maandalizi hayo.

 

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, ameliambia Spoti Xtra kuwa, leo Jumapili, wachezaji wote wa Simba wataingia kambini, kisha kesho Jumatatu wataanza mazoezi.

 

“Mazoezi ya Simba yanatarajia kuanza rasmi Jumatatu kwa wachezaji wote kufi ka kambini kwa wakati tayari kwa kuanza msimu mpya, kocha pia aliondoka, lakini Jumatatu anatarajia kuwa na kikosi tayari kwa kuanza maandalizi ya msimu mpya.

“Kila kitu kinakwenda sawa, wachezaji wote waliotambulishwa nimewapokea ambao wote wanatarajia kuanza mazoezi Jumatatu,” alisema Rweyemamu.Wakati huohuo, Morrison amewatumia salamu mashabiki wa Simba na kuwataka kuwa watulivu na kumuunga mkono kwani amekuja kuyafanya makubwa kwenye timu yao.

 

Morrison alitumia ukurasa wake wa Instagram kuwajuza mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuwa alizungumza na mwekezaji wa klabu hiyo Mohamed Dewji na kumuahidi kuwa atatulia na kufanya makubwa ndani ya timu hiyo.Mbali na hilo, Morrison alifunguka kuwa alipokuwa anafanya kazi ndani ya Yanga, walishindwa kumpa thamani na kumuona kuwa kama mchezaji asiye na nidhamu na mtukutu jambo ambalo halikuwa la kweli.

 

“Nimemaliza kuzungumza na bosi wangu wa Simba SC (Mo Dewji) na kumuahidi kuwa nitakuwa mfano mzuri, kuheshimu klabu na wanachama wake na kucheza kwa juhudi ili kila mtu afurahi.

 

“Nimefanya kazi na Yanga kwa miezi minne, waligundua kuwa mimi ni kijana mbaya na sina nidhamu wakati nilipotaka kuondoka, lakini mimi sina tatizo lolote dhidi ya mtu yoyote.

 

“Kwa wapenzi wa Simba nipo pamoja na nyinyi, niko hapa kuwafanya mfurahi, niko hapa kuwaheshimu na kuwawakilisha kwa njia yoyote ile, sahau yanayosemwa kuhusu mimi, nawaacha, tufanye kazi,” alisema Morisson.

STORI: KHADIJA MNGWAI NA ISSA LIPONDA,Dar es Salaam

Leave a Comment