MSHAMBULIAJI ambaye aliwaua kwa bunduki waumini 51 kwenye misikiti miwili nchini New Zealand amehukumiwa kifungo cha maisha jela na kwa sharti kwamba muda wa kifungo hicho hauwezi kupunguzwa.
Jaji Cameron Mander amesema hukumu hiyo ambayo ndiyo ya juu zaidi na ya kwanza kutolewa nchini New Zealand, inalenga kuonyesha jinsi matendo ya mshambuliaji huyo Brenton Tarrant yalivyokosa utu.
Mander ameongeza kuwa makosa yaliyofanywa na mwanamme huyo raia wa Australia ni ukatili wa kiwango kibaya ambao hata hukumu ya maisha jela haiwezi kufuta hasara na maumivu aliyosababisha.
Katika mashambulizi ya Machi 2019, Tarrant aliwashambulia kwa bunduki za rashasha waumini waliokuwa kwenye ibada katika misikiti ya Al Noor na Linwoood mjini Christchurch.
Tangu Machi mwaka huu Tarrant alikubali mashtaka hayo yaliyokuwa yakimkabili na kusema anakiri kuwa na hatia ya kuwaua waumini 51 na jaribio la kuwauwa wengine 40 katika mashambulizi ya bunduki aliyoyafanya mwezi Machi mwaka 2019.
