MGOMBEA Urais Visiwani Zanzibar, Dkt Hussein Mwinyi na Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt Magufuli wote kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa pamoja wamefanya Kampeni visiwani Unguja Zanzibar ambapo wameewaeleza wananchi vipaumbele watakavyo hakikisha wanavitimiza.
“Miaka 135 iliyopita baadhi ya mataifa makubwa ya Ulaya yalikutana Berlin, Ujerumani na kuligawana Bara la Afrika vipande vipande na kuanza kulitawala, machungu ya kutawaliwa tunayajua kama hatukuyaishi, basi tumesimuliwa na mababu zetu.
“Muungano wetu sio wa kulazimisha ni wa hiari, ni maono ya mbali ya waasisi wetu, ukaribu wa kijiografia kati ya Zanzibar na Tanganyika, mahusiano ya kindugu na kirafiki yaliyochagizwa na Lugha ya Kiswahili, ukaribu wa vyama vilivyopigania uhuru (TANU & ASP).”
“Ukimsikia mtu anasema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni wa kulazimishwa basi huyo ni mzushi na hajui vizuri kuhusu muungano huo, na mtu wa namna hiyo hapaswi kabisa kupewa nafasi ya kuliongoza Taifa.
“Wananchi wa Zanzibar na Tanganyika walikuwa na muingiliano wa kindugu kabla hata ya kuja kwa Wakoloni, ndiyo maana huku Zanzibar wapo akina Makungu, kule usukumani maana yake ana uwezo sana, kule Bara nako kuna akina Makame, hiyo ndiyo Tanzania.
“Kufuatia kuibuka kwa Corona sisi tumeonyesha ni Taifa huru. Mataifa yote Duniani yalielekezwa kufungia watu wake ndani, sisi tulikataa kupokea maelekezo hayo, tukaamua kumtanguliza Mungu, tulikataa kuwa ‘dodoki kavu’ linalosomba kila uchafu.
“Mkifungua TV mnaona watu walivyofunga pua zao na midomo yao, akipiga chafya hata mkeo unamkimbia chumbani, ni mateso, sisi tulisema tunamtanguliza Mungu na Corona ikatokomea, Mungu amefanya maajabu, Mungu Oyee!.” – Dkt. Magufuli, Zanzibar.
“ZECO ilikuwa inadaiwa Tsh bilioni 22.9 na TANESCO, nililifuta hilo deni nikasema hazilipwi kwa sababu Zanzibar ni Tanzania na Tanzania ni Zanzibar, huwezi kuwatwisha zigo hilo Wazanzibar wakati umeme huu wote unatoka Tanzania, hii ni raha ya Muungano.
“Katika kipindi cha miaka kama 40 zimekopwa fedha na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya miradi ya Zanzibar pekee yake fedha zenye thamani ya Trilioni 2.3.
“Mwinyi namuita kijana kwa sababu namzidi umri, amekuwa waziri kwa miaka 20 na mimi nilikuwa waziri kwa miaka 20 kabla ya urais, amekuwa Waziri wa Ulinzi miaka 11, vifaru vinamjua, mizinga inamjua lakini hakuwa na tamaa ya kupindua Serikali, ana moyo wa kipekee.
“Ndugu zangu Wazanzibar watu wazuri huwa hamuwajui, kule Pemba kulikuwa na Prof Mbarawa amegombea wee wanamnyima, nikamchukua nikampa Wizara ya Ujenzi akafanya kazi vizuri, kukawa na matatizo Wizara ya Maji nikampeleka amefanya vizuri, Pemba hawajui ile ni dhahabu.
“Utamlinganisha Mwinyi na waliogombea miaka 25 iliyopita? Kila baada ya miaka mitano unagombea, uligombea na babu yako ukaja kugombea na wajukuu, Wazanzibar wanataka maendeleo, mchagueni Mwinyi, na wewe ukichaguliwa hakikisha Makamu wa Pili wa Rais anatoka Pemba.
“Mwinyi amekuwa Waziri wa Ulinzi miaka 11, mizinga yote inamjua, vifaru vyote vinamjua, helikopita za vita zote zinamjua, mabomu yote yanamjua, Baba huyu hakuwa na tamaa hata ya kupindua Serikali, ana moyo wa uvumilivu.”
“Nimekuwa Waziri wa Uvuvi na Mifugo, nikapeleka Sheria ya Deep Seas Fishing Authority, nikapendekeza makao makuu ya uvuvi kuwa Zanzibar, mtu gani anaweza akasema hamtaruhusiwa kuvua? Ni wachonganishi, washindwe na wakalegee.
“Najiuliza sasa hivi nikichaguliwa kuwa rais nitapata shida kumtafuta Waziri wa Ulinzi kama Hussein Mwinyi, sasa ninashangaa huku wapo baadhi ya watu wanasema hawezi, mavifaru yalimheshimu ashindwe kuongoza hii nchi.
