
Benki ya Exim Tanzania imeungana na ulimwengu wote kwa kutoa heshima kwa wateja na wafanyikazi wa benki hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Kimataifa ya Huduma kwa Wateja inayofanyika kila mwaka mwezi Oktoba. Benki hiyo imeahidi kuboresha zaidi huduma zake hususani zile za kidigitali.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Bwana Jaffari Matundu akiwa ameambatana na maofisa waandamizi wa benki hiyo walitembelea matawi kadhaa pamoja na baadhi ya wateja wa benki hiyo jijini Dar es Salaam ili kuzungumza na wafanyakazi pamoja na kupata mrejesho kutoka kwa wateja wa kuhusu huduma zinazotolewa na wateja wa benki hiyo.

“Kama taasisi inayotoa huduma muhimu kwa wateja, wiki hii ni muhimu kwetu Benki ya Exim kwa kuwa inatupa fursa ya kushirikiana kikamilifu na wateja wetu. Uhusiano mzuri na madhubuti na wateja wetu unabaki kuwa muhimu sana kimkakati na hatua hii inaonyesha nia yetu ya kutambua jambo hili, ”alisema Bw Matundu wakati alipotembelea tawi la Makao Makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam leo.
Akizungumzia umuhimu wa utoaji wa huduma kwa ubora, Bw Matundu aliwapongeza wafanyakazi wa benki hiyo huku akionyesha kutambua namna wanavyojituma kuwahudumia wateja kwa weledi na kwa uaminifu mkubwa.

“Kila wakati tumekuwa tukitafuta njia mpya za kuwahudumia wateja wa benki ya Exim kwa weledi zaidi huku pia tukihamasisha ukuaji wa pamoja kati yetu na wateja wetu.” Alisema.
Kwa upande wake Meneja Mwandamizi wa Huduma kwa Wateja wa benki hiyo Bwana Frank Matoro alifafanua namna benki hiyo inavyojitoa katika kuwahakikishia utoaji wa huduma bora wateja wake ili kukidhi mahitaji na matarajio yao wakati wote.

“Ni muhimu kuonyesha na kuthamini thamani ya utoaji bora wa huduma kulingana na uzoefu na mahitaji ya wateja wetu, kwa kuwa vitu hivi ni viungo muhimu katika kujenga taasisi ya kifedha yenye nguvu zaidi nchini.” Alisema.

Katika ziara yake kwa baadhi ya wateja wa benki hiyo jijini Dar es Salaam huku akiwa ameambatana na baadhi ya maafisa waandamizi wa benki hiyo Bw Matoro alitumia fursa hiyo kutumia na kuelezea baadhi ya huduma zinazotolewa na benki hiyo hususani zile za kidigitali yakiwemo matumizi ya kadi za benki katika kufanya miamala.

“Ili kufanya huduma zetu ziwe nzuri zaidi na rahisi kwa wateja, Exim benki tunazo chaguzi kadhaa ikiwemo kutumia huduma ya mobile bank inayohusisha matumizi ya simu za mkononi au kwa njia ya USSD, kutumia kadi zetu za benki, mtandao wetu wa POS na pia kutumia huduma za mtandaoni kupitia wavuti au programu (App) ambazo zinawawezesha wateja wetu kupata huduma muhimu za kifedha muda wote ,’’ alitaja Bw Matoro.

Kufuatia ziara hizo baadhi ya wateja wa benki hiyo ikiwa ni pamoja na kampuni za MMI Tanzania, inayojishughulisha na biashara ya mvinyo pamoja na kampuni ya Shrijee Traders walionesha kuridhishwa kwao na huduma zinazotolewa na benki hiyo pamoja na heshima ya kutembelewa na maofisa wa benki hiyo.

“Kimsingi nimekuwa nikiridhishwa na huduma ninazopatiwa kupitia benki ya Exim ikiwemo malipo ya hundi, malipo kwa njia ya mtandao pamoja na matumzi ya kadi za malipo ambayo kiukweli zinatolewa kwa ufanisi mkubwa. Niwaombe tu benki ya Exim waendelee kuhamasisha malipo kwa njia ya kidigitali maana ni bora zaid.Ninajivunia kuhudumiwa na Benki ya Exim,’’ alisema Bw Sabalsinh Champs, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Shrijee Traders inayomiliki Supermarket ya Shrijee’s iliyopo jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam: OKTOBA 7th, 2020