POLISI Mkoa wa Mbeya inamshikilia Salome Mbuya (23) Mkazi wa Mnazi kwa Ndomba wilayani Mbarali kwa tuhuma za kumjeruhi vibaya sehemu ya shingoni Tabia Abdallah (38) Mkazi wa Msesule kwa kumchoma kisu sehemu ya shingoni upande wa kisogoni na kupelekea kupoteza fahamu.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich O. Matei, inasema mtuhumiwa alifanya hivyo akimtuhumu Tabia kumtangaza yeye na wenzake pindi wakichepuka nje ya ndoa zao.
Inadaiwa tukio hili lilitokea Oktoba 6, 2020 Kijiji cha Mnazi, Kata ya Imalilosongwe, Tarafa ya Ilongo, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya.
Aidha taarifa hiyo inasema polisi inamshikilia Masunga Yanora (35) ,kazi wa Bariadi Mkoa wa Simiyu kwa tuhuma za kumvamia na kumjeruhi kwa kumpiga fimbo Sikujua Mayenga (30) mkazi wa Mpembe Pepea na kumjeruhi sehemu ya kichwani, kifuani na mbavu za kushoto.
Taarifa inasema hilo lilitokea Oktoba 7, 2020, Kitongoji cha Mpembe, Kijiji na Kata Lualaje, Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya. ambapo Sikujua alivamiwa nyumbani kwake na watu watatu ambao aliwafahamu kwa sura waliokuwa na fimbo na kumjeruhi kichwani, kifuani, mbavu za kushoto na baada ya tukio hilo watuhumiwa hao walitokomea kusikojulikana.
Polisi lilifanya msako na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa Masunga aliyekiri lengo lake lilikuwa ni kumuua Kija Malimu mume wa Sikujua lakini baada ya kumkosa ndipo wakamshambulia mke wake.
Mtuhumiwa anadai aliitwa na Juma Masanja mkazi wa Lualaje Wilaya ya Chunya ili amuua Kija kwa ujira wa Tshs 3,000,000 kutokana na wivu wa kimapenzi ambapo Juma alimtuhumu Kija kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mke wake.
Upelelezi unaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine waliohusika kwenye tukio hili.
Pia polisi mkoani humo inamshikilia Samson Kyando (26) mkazi wa Mswiswi Wilaya ya Mbarali kwa tuhuma za mauaji ya mke wake aitwaye Cecilia Wilson (24) kwa kudaiwa kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia majeraha hali iliyosababisha kupelekwa Hospitali ya Misheni Chimala kwa matibabu na hatimaye kufariki Oktoba 6, 2020.
Chanzo cha tukio hilo kinasemekana ni ugomvi wa kifamilia baina ya marehemu na mtuhumiwa.
Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
