×

Nina Moto Mkali na Dar, Itakuwa ya Ma-Flyover Tu – Video

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Dkt. John Magufuli, leo Oktoba 09, amefanya mkutano wa kampeni jijini Dar es Salaam katika Uwanja wa Mkapa ambapo kampeni hizo zimepambwa na burudani kutoka kwa wasanii wa nyumbani akiwemo, Diamond Platnumz, Harmonize, Alikiba, Maua Sama, Dulla Makabila, Nandy na wengine wengi.

 

Akizungumza wakati wa mkutnao huo, Magufuli amesema; “2015 tuliwaambia tutaibadili Dar es Salaam watu hawakuamini, leo ninyi ni mashahidi tumeibadilisha Dar es Salaam, na bado awamu hii tutaibadilisha zaidi. Tumejenga zaidi zaidi ya kilometa 200 za lami kwa jiji la Dar, tumetumia zaidi ya Tsh bilioni 660, nyie ni mashahidi, Barabara ya Morocco, Shekilango, barabara ya njia nne ya Kimara – Kibaha.

 

”Nimesikia mgombea mmoja akilalamika tunajenga barabara pana ya njia nane, yeye ametembea hajawahi kuona barabara ya hivi, kule Houston kuna barabara yenye njia 26, hakuna ubaya sisi tukiwa na kitu kikubwa dunia nzima Mungu alitupa Mlima Kilimanjaro, mrefu kuliko yote.

 

”Tulipoingia madarakani mwaka 2015, vitendo vya uhalifu na ujambazi vilikuwa vimekithiri sana, mtu alikuwa akienda benki kuchukua pesa zake anakuwa na wasiwasi atavamiwa, maeneo ya Rufiji, Kibiti na Mkuranga wahalifu walikuwa wakijificha kule, lakini tumewadhibiti mno.

 

”Tumepanga kukamilisha mradi wa mabasi ya Mwendokasi kutoka Kariakoo Gerezani mpaka Mbagala ili watu wa Mbagala nao waanze kunufaika na mradi huu.

 

”Dar es Salaam itakuwa na ma-flyover mengi mno, pale makutano ya Chang’ombe, Uhasibu, kamata, Morocco, Mwenge, Magomeni, Tabata, Fire, Makutano ya Ali Hassan Mwinyi, Umoja wa Mataifa na Kinondoni, tunajenga pia daraja la Mzinga, Wazaramo watachagua daraja la kufungia ndoa

 

”Katika wilaya mpya ambazo miundombinu ya barabara haijawa nzuri sana, maeneo flani ya Ubungo na Kigamboni, hata Ilala tumejipanga vizuri sana kutengeneza barabara za lami mtu akiambiwa atafute barabara ya changarawe aikose Dar es Salaam, nataka niibadilishe Dar.

 

“Nchi yetu inapakana na nchi nane ambapo nchi sita hazina bandari hivyo kutegemea bandari ya Dar es Salaam. Na hii inaonyesha jinsi gani Dar es Salaam inachangia pato la taifa. Wajasiriamali tembeeni kifua mbele, Serikali ya Magufuli iko pamoja na ninyi, haitawaacha na wala hamtabugudhiwa na mtu yoyote. Na yule anayetamani kuwabugudhi ashindwe na akalegee potepote.

 

“Mabasi ya mwendokasi yamepunguza kero ya foleni kwa kiasi kikubwa kwa wakazi wa Kimara, safari ambayo ilikuwa inachukua saa tatu (3) hadi nne (4) sasa wanatumia dakika 45 tuu. Miradi inayoendelea ni uchimbaji wa visima virefu vya mpiji na mpera vyenye thamani ya Bilioni 18.9.

 

“Jiji hili lina idadi kubwa ya watu kuliko majiji yote. Takwimu zinaonyesha mpaka kufikia 2030 litakuwa na watu 10 milioni. Tumenunua ndege 11 ambapo katika miaka mitano kama mkitupa ridhaa tumepanga kununua ndege nyingine 5 moja ikiwa ni ya mizigo.

 

“Bajeti ya madawa imeongezeka kutoka Billioni 11.2 mwaka 2015/2016 hadi bilioni 18 mwaka 2019/2020. Tumejenga hospitali za wilaya 4, vituo vya Afya 10 na zahanati 14. Tumeimarisha pia huduma za jamii hususani Afya, maji, elimu na umeme. Samabamba na hayo tumepeleka vifaa tiba vya kisasa Muhimbili, Moi na Jakaya Kikwete.

 

“Tumeanza ujenzi wa reli ya kisasa Dar es Salaam yenye urefu wa 700km yenye thamani ya Trilioni 7.062. Jana nimeshuhudia kuwekwa jiwe la msingi la mradi wa Stand kubwa ya mabasi pale Mbezi Louis.” – Dkt. Magufuli.

 

Nataka watu wakitoka Ulaya wakashuka Dar es Salaam wajue kama bado wako Ulaya, bado nina moto mkali na Dar es Salaam, mwili wangu unawasha washa kuiletea maendeleo Dar es Salaam, tumepanga kufanya mabadiliko makubwa, tunataka tuimarishe hospitali zaidi Jakaya Kikwete mioyo iwe inapasuliwa “usiku na mchana, watu wawe wanatoka Ulaya wanakuja huku siyo kwenda huko,” amesema Magufuli.

 

Leave a Comment