×

The Angel Of Darkness-23

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anaokotwa na vikosi vya uokoaji na kurejeshwa Tanzania wakati Brianna anaokotwa na mwanamke mwendawazimu, Mashango na kwenda kuishi naye kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge, Mathare jijini Nairobi baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari. Anapohitimu darasa la saba, anakosa mtu wa kumlipia masomo ya sekondari na kusababisha arudie kwenye biashara aliyokuwa anafanya na marehemu Mashango ya kuuza mbogamboga na matunda.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anauza kinyemela nyumba aliyoachiwa na wazazi wake na kutorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kipekee ya kukutana na mfanyabiashara mkubwa wa madini ya Tanzanite ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake. Wanakubaliana wamdanganye mfanyabiashara huyo kwamba Arianna na Diego walikuwa ndugu wa damu wakati ukweli ni kwamba wawili hao ni wapenzi.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Ila tuache masihara Arianna, unajua mwenzio najisikia wivu sana.”
“Wivu wa nini?”
“Naona kama mwisho wa siku unaweza kuacha kunipenda mimi ukakolea kwa Msuya maana anakujali sana na ananizidi kwa kila kitu,” alisema Diego huku akionesha kumaanisha kile alichokisema, Arianna akacheka sana na kumtoa wasiwasi kwamba hata iweje kamwe hawezi kuachana naye.

Muda ulizidi kuyoyoma na hatimaye jioni ikawadia, kama Msuya alivyokuwa ameahidi, alimpigia simu Arianna kwa kupitia simu ya Diego na kumueleza kuwa tayari ameshafika sehemu wanayokutania kila siku, akamuomba ajikaze na kwenda kuonana naye ili ampe mzigo wake.

Japokuwa kwa muda wote Arianna alikuwa akipiga stori na Diego, alipopigiwa simu tu, alivaa uso wa huzuni kuonesha kwamba kweli alikuwa anaumwa, akajitanda khanga, jambo ambalo halikuwa kawaida yake na kutoka mpaka nje ambapo alimkuta Msuya akiwa amepaki gari lake la kifahari, pembeni kidogo na pale wawili hao walipokuwa wanaishi.
Arianna alipofika, mwanaume huyo alimpokea kwa bashasha za hali ya juu, akamfungulia mlango wa gari lake na kuanza kuzungumza naye, huku Arianna akiendelea kujifanyisha kwamba anaumwa sana.

”Sasa kwa sababu unatumia dawa za Malaria, naomba nikupeleke hapo jirani kuna hoteli nzuri wanapika vyakula vinavyoweza kukufaa. Ukipata supu ya kuku nadhani itakufaa sana kwa sababu unatumia dawa,” alisema Msuya kwa sauti ya upole, Arianna akatingisha kichwa kuonesha kukubaliana naye.

Akawasha gari na kuelekea kwenye hoteli ndogo lakini yenye hadhi ya juu iliyokuwa jirani na pale Arianna alipokuwa anaishi na Diego, wakatafuta sehemu tulivu na kukaa, Msuya akamuita mhudumu na kumtaka amsikilize Arianna.
Muda mfupi baadaye, supu ilikuwa mezani sambamba na boksi kubwa la juisi, huku muda wote Msuya akimsisitiza Arianna ale kwa sababu alikuwa anaumwa. Kwa jinsi mwanaume huyo alivyokuwa akimjali Arianna, alijihisi kuwa mwanamke wa kipekee sana chini ya jua.

Walipomaliza, Msuya aliinuka na kwenda kwenye gari, akashuka na kiboksi ambacho hata bila kuuliza, Arianna alijua kuwa lazima ndani yake kuna simu aliyoahidiwa. Msuya akarejea na kukaa karibu na Arianna, akampa kiboksi na kumtaka mwenyewe afungue ajionee kilichokuwa ndani.

“Whaooo! iPhone 4s? Siamini macho yangu,” Arianna alipiga kelele kwa furaha kiasi cha kuwashtua wateja wengine waliokuwa wamekaa pembeni yao ambapo walianza kuwatazama. Kitendo cha kupewa simu hiyo ya kifahari kilimfurahisha mno Arianna kwani kwa wakati huo, hiyo ndiyo simu iliyokuwa ikiuzwa ghali pengine kuliko simu zote, ikiwa na vitu vingi vya kisasa.

Kwa jinsi Arianna alivyofurahi, alijikuta akiinuka na kumkumbatia Msuya kwa nguvu, akambusu shavuni, jambo ambalo lilimfurahisha sana mwanaume huyo. Akamsaidia kuiwasha na kuanza kumuelekeza namna ya kuitumia kisha baada ya hapo, alimrudisha mpaka jirani na walipokuwa wakiishi na kuagana naye.

Kama kawaida, kabla hajaondoka, aliingiza mkono kwenye mfuko wa suruali yake, akatoa ‘waleti’ iliyokuwa imenona kiasi cha kushindwa kufungika vizuri, akahesabu noti kadhaa na kumpa Arianna, akambusu kwenye paji la uso na kumtakia heri apone haraka. Arianna akaondoka taratibu huku mwanaume huyo akimsindikiza kwa macho mpaka alipozamia uchochoroni.

Diego alishindwa kuamini macho yake wakati Arianna akimuonesha simu hiyo muda mfupi baada ya kuingia ndani, akitoka kuonana na Msuya. Ile hali ya wivu ikazidi kumtesa ndani ya moyo wake kwani aliamini kwa jinsi mwanaume huyo alivyokuwa anamhudumia Arianna, upo uwezekano mkubwa akaangukia kwenye penzi lake na kumuacha Diego akiwa hana cha kushika.

Siku hiyo ilipita, ukaribu kati ya Msuya na Arianna ukazidi kuwa mkubwa, mara kwa mara Msuya akawa anampigia simu Arianna, kumtumia muda wa maongezi na wakati mwingine kumtumia meseji nzuri za kimapenzi. Upendo aliokuwa akioneshwa na Msuya, ulimfanya Arianna aanze kuwa na furaha kwenye maisha yake, muda mwingi tabasamu pana likawa linaupamba uso wake na kumfanya azidi kuonekana mrembo.

Hata matumizi ya madawa ya kulevya alipunguza kidogo japokuwa hakuweza kuacha, muda wote akawa anatamani akae na Msuya akiwa na akili zake timamu. Kingine kilichomfurahisha zaidi, Msuya hakuonesha kuwa na haraka ya kufanya naye mapenzi kwani kwa kipindi chote tangu walipokutana, alikuwa akimhudumia kwa kila kitu lakini hakuwahi kugusia suala la kukutana kimwili.

Siku zilizidi kusonga mbele, hatimaye Arianna na Diego wakahamia nyumbani kwa Msuya.
Kama walivyokuwa wamekubaliana, Arianna na Diego waliendelea kuitana kaka na dada na kuwekeana nadhiri ya kufanya kila kinachowezekana ili kumfanya kila mtu aamini kwamba wawili hao walikuwa ni ndugu wa baba na mama mmoja.

“Arianna!”
“Abee.”
“Najua itakuwa vigumu sana kwako kuamini kwamba nakupenda kwa dhati na lengo langu siyo kukutumia bali ni kuishi na wewe maisha yangu yote,” alisema Msuya kwa sauti ya upole, jioni ya siku Arianna na Diego walipohamia kwenye jumba la kifahari la mfanyabiashara huyo.

Msuya aliendelea kuzungumza kiutu uzima kwa sauti iliyokuwa imejaa mahaba na kumwambia Arianna kwamba kwa sababu amekubali kuhamia nyumbani kwake, inabidi wafanye taratibu zote za kisheria ili wafunge ndoa na hatimaye kuishi kama mume na mke.

“Inabidi ujiandae twende hospitali tukapime afya zetu kisha baada ya hapo tuanze kufanya taratibu za kufunga ndoa,” alisema Msuya, kauli ambayo iliupasua moyo wa Arianna kama mkuki wenye ncha kali.
Nyendo zake na aina ya maisha aliyoishi tangu alipovunja ungo, vilimfanya Arianna awe na wasiwasi mkubwa juu ya afya yake kwani kipindi alipokuwa akianza kutumia madawa ya kulevya, alikuwa akilewa na ‘kuzimika’, hali iliyokuwa inasababisha wanaume wengi kumuingilia kimwili, tena bila tahadhari yoyote. Pia hakumuamini kabisa Diego kutokana na nyendo zake.

“Vipi mbona kama umezama kwenye mawazo? Nimekuudhi?” alihoji Msuya baada ya kumuona Arianna amebadilika, kauli hiyo ndiyo iliyomzindua msichana huyo mrembo kutoka kwenye dimbwi la mawazo, akashtuka na kukaa vizuri.

Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

1 Comment

Leave a Comment