×

Mapazia ya Chumbani -14

Aliona kama miujiza kurudi kwa mumewe akiwa amelewa. Aliingia chumbani na kuzima taa kisha akamfuata mzee Mashali na kuanza kuingiza taratibu kwenye mifuko yake ya suruali na kutoka na simu.

Akafunga mlango kwa funguo na kuelekea kwa mama Muro kukamilisha mtego.

ENDELEA NAYO MWENYEWE…

Akili yote ya mama Dick ilikuwa nikufika kwanza kwa shoga yake, mama Muro kukamilisha mtego waliokuwa wamepanga kuufanya.

“Huyu Mungu!! Wee acha aitwe tu Mungu,” alijisemea peke yake akipiga hatua chache kukaribia kwa mama Muro.

“Hodi humu jamani, mama Muro!” aliita mama Dick.

“Niko jikoni huku pitiliza moja kwa moja.”

Mama Dick alifuata maelekezo kama alivyokuwa ameambiwa na mama Muro mpaka jikoni.

“Kulikoni mbona unahema juujuu au umeshalikoroga hakuna dili tena?”

“Wee!! Kusiwe na dili tena? Embu twende kwa kule mbele kibarazani nikuambie.”

Mama Muro alitelekeza hilo na kwenda hadi kibarazani.

“Kwanza vipi ameshakuja yule kijana?”

“Bado lakini ndiyo muda wenyewee huu, niambie basi maana unavyonipa mshawasha!”

“Nimefanikiwa mwenzako na simu hii hapa!”

Mama Muro alishtuka, alitoa macho mithili ya mjusi kabanwa na mlango.

“Hee embu nisimulie kwanza shemeji umemuacha wapi?”

Mama Dick hakutaka kuongea chochote zaidi ya kufungua pindo la kanga yake na kutoa ufunguo wa nyumbani kwake kisha akamuonesha mama Muro.

“Kwahiyo unataka kusema shemeji hayupo nyumbani?”

“Yupo na nimemfungia.”

“Shoga weweee, umempa nini?”

“Chezea mtoto wa Kitanga tena! Halooo!!. Hakuna mwaya nakutania, limekuja zake likiwa limelewa tiii, nikaliandalia chakula, likasema limeshakula lilipotoka, basi likajibwaga kitandani na hapo ndiyo ukawa mwanya wangu wa kuichukua simu na kuja hapa.”

“Sasa akishtuka kwa bahati mbaya!”

“Hivi shoga, mtu aliyelewa huwa anajitambua anachofanya na kukisema?”

“Hapana!”

“Basi elewa kuwa hawezi kufanya lolote.”

Mama Muro bado alikuwa hataki kuamini kama mama Dick ameweza kufanikiwa kirahisi kiasi kile. Aliichukua ile simu aliyokuwa nayo mama Dick na kuiangalia vizuri.

“Umeamini sasa,” alisema mama Dick.

“Duuh we balaa, haya iwashe basi!”

Mama Dick aliichukua na kuiwasha ikawaka na baada ya sekunde kadhaa ikajiloki. Ikahitaji namba za siri ili iweze kufunguka.

“Duhh! Kwahiyo hufahamu namba za siri alizokuwa akizitumia,” alisema mama Muro kwa kukata tamaa.

 “Nifahamu wapi miye, kwanza mzee Mashali huwa ni mkali sana mtu akishika simu yake.”

Wakiwa katika kuwaza na kuwazua mara yule kijana waliokuwa wamepanga naye mikakati ya kumkabili mama Kirumba akawa ameshafika.

“Salama jamani!”

“Uko sawa na muda, ndivyo inavyotakiwa na ulivyojipamba safi sana utasema siyo kijana,” mama Muro alimsifia.

“Sasa, ndiyo nimekuja kikazi zaidi si unajua hapa kazi tu!”

“Embu acha kutuchekesha! Tumefanikiwa kwa kiasi kikumbwa kukamilisha hatua tutakazozifanya lakini kinachotutatiza hapa ni hii simu.”

“Simu? Imefanyaje kwani?”

“Si unajua ili tukamilishe ule mtego niliokuambia ni lazima matumizi ya simu yahusike kwa kiasi kikubwa kati ya wewe na huyo mama na tena si unaona nyumba ile pale.”

“Ndiyo pale.”

“Ndiyo. Embu tujadiliane ni jinsi gani tunaweza kutumia hii simu ya mume wake na huyu shoga yangu anayeibiwa mume na mwanamke wa nyumba ile pale.”

“Kwa hiyo tatizo kubwa la simu ni nini?”

“Hii simu inataka namba za siri ili iweze kutumika na namba hizo za siri huyu mkewe hazijui.”

“Mbona rahisi tu!”

“Kweli? Kivipi maana hapa tulipo tumechanganyikiwa na tunachotaka kukifanya ni jinsi ya kuweza kuwasiliana kupitia simu hii.”

“Simu yangu hii hapa cha muhimu leteni hiyo laini ya hiyo simu niingize kwangu nifanye kazi iliyonileta.”

Mama Muro na Mama Dick wakaangaliana. Hawakuwa na wazo jepesi la namna hiyo, walimpa laini ya simu ya mzee Mashali na kuiweka kwenye simu tayari kwenda kukamilisha mtego walioupanga.

“Cha kwanza chukua namba za simu za huyo mama,” alisema mama Dick na kuitoa simu yake tayari kumpatia namba. Kitendo cha kuiandika ile namba jina likajitokeza moja kwa moja kwenye ile simu likiwa limeandikwa Mpaka Chumbani.

“Hee makubwa!” aliropoka mama Muro baada ya kuliangalia lile jina.

“Kwa hiyo hakuna kulemba, tunataka na meseji ya kwanza umtumie tukiwa wote hapa,” alisema  mama Dick.

Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye gazeti hilihili Jumanne ijayo.

Leave a Comment