×

Meneja Kampeni Mgombea Ubunge Afariki, Chanzo Hiki Hapa…

POLISI mkoani Mwanza wanachunguza chanzo cha kifo cha Deogratias Medard (42) mkazi wa Sengerema aliyefariki dunia muda mfupi baada ya kudaiwa kula makande na chai akiwa kwenye kampeni za mgombea ubunge jimbo la Sengerema kwa tiketi ya CCM, Hamis Tabasamu,  ambapo marehemu alikuwa meneja wake wa kampeni.

 

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kifo cha Medard, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro alisema, tukio hilo lilitokea majira ya saa 12:35 jioni katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Sengerema.

 

Alisema marehemu kabla ya kufikwa na mauti alilalamika kuumwa tumbo baada ya kula chakula hicho na akalazimika kukimbizwa hospitali lakini alipoteza maisha kabla ya kupata tiba.

 

Muliro alisema  jeshi hilo linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha kifo hicho kama kimesababishwa na sumu na ni sumu aina gani.

 

Mbali na uchunguzi pia linaendelea na mahojiano na watu kadhaa waliokuwa na marehemu kwenye kampeni kabla ya kifo.

 

Aidha jeshi hilo mkoani humu limesema limejipanga vizuri kuelekea uchaguzi mkuu na kuwataka wananchi wajitokeze kupiga kura Oktoba 28, bila hofu.

Leave a Comment