×

Adaiwa Kuua Mke, Shemeji kwa Shoka

JESHI la Polisi mkoani Kagera linamshikilia mtuhumiwa Faraji Yunus (44), mkazi wa Kijiji cha Kikagati wilayani Muleba mkoani Kagera, kwa tuhuma za mauaji ya mkewe na shemeji kwa shoka. 

 

Yunus anadaiwa kuwaua mkewe, Nadia Coroneli (35) na shemeji yake, Shadia Yunusu (25), wakazi wa kijiji hicho.

 

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi, alisema kuwa Oktoba 29, mwaka huu majira ya saa 12 jioni, mtuhumiwa akiwa kijiji hapo alisababisha ugomvi uliosababisha mauaji hayo.

 

Alisema, mtuhimiwa alipata taarifa kuwa mkewe alikuwa akifanya usaliti wa ndoa na kufikia hatua ya kutaka kwenda kuolewa sehemu nyingine, hivyo mtuhumiwa kuanza matukio ya kuzua ugomvi.

 

“Alipopata taarifa hizo alianza ugomvi na mkewe, ambao ulipelekea kumuua mkewe  Nadia na Shadia Yusuph, mke wa mdogo wake Yusuf  Yunusu kwa kutumia shoka,” alisema Kamanda Malimi.

 

Aidha, alisema akiwa katika ugomvi huo, alifika mtu ambaye mtuhumiwa alikuwa akidai kuwa ana mahusiano na mkewe, na kutaka kuamulia ugomvi huo.

 

Kamanda alisema mtuhumiwa alimuua shemeji yake kutokana na kumtuhumu kuwa alikuwa anamtafutia mabwana mkewe, huku akijua kuwa ni mke wake wa ndoa.

 

Alisema baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alijaribu kukimbia lakini juhudi za polisi wilayani Muleba ziliwezesha kukamatwa na kufikishwa kituoni. Alisema, upelekezi wa tukio unaendelea ili kubaini sababu zaidi kabla ya kufikishwa mahakamani.

Leave a Comment