NOVE MBA 7 ilikuwa ikisubiriwa kwa shauku kubwa na wadau wa soka nchini ili kushuhudia pira biriani kwa timu mbili ambazo ni Yanga na Simba ndani ya Uwanja wa Mkapa, hatimaye imewadia.
Timu hizo zinakutana zikiwa zimesheheni mastaa wakubwa wenye uwezo wa kusaka matokeo ndani ya uwanja ambapo kwa Yanga wana mshambuliaji Michael Sarpong raia wa Ghana mwenye mabao mawili huku Simba nguzo yao ikiwa ni kiungo Clatous Chama raia wa Zambia.
Ndani ya misimu saba mfululizo wakiwa wamekutana mara 14, sawa na dakika 1,260 wakiwa wameziyeyusha uwanjani jumla ya mabao 25 yamefungwa ambapo ni wastani wa bao moja kila baada ya dakika 50.
Yanga imeshinda jumla ya mechi tatu na Simba imeshinda mechi nne huku sare zikipa tikana mara saba.
Championi Ijumaa inakuletea rekodi za mechi zao 14 zilizopita pamoja na wafungaji wa mabao hayo mambo yalikuwa namna hii.
2013/14
Oktoba 20, 2013, Yanga 3-3 Simba
Wasome waliopeleka maumivu kwa Simba ni Mrisho Ngassa dakika ya 15 na Hamis Kiiza, yeye alitupia mabao mawili dakika ya 35 na 45.
Waliopindua meza kwa upande wa Simba ni Bertram Mombeki, dk 54 Joseph Owino 58 na Gilbert Kaze dakika ya 85.
Walipokutana Aprili 19, 2014, ngoma ilikuwa Simba 1-1 Yanga. Kwa Simba ni Haruna Chanongo aliyetupia bao dakika ya 76 na kwa Yanga Simon Msuva dakika ya 86.
2014/15
Oktoba 18, 2014, Simba 0-0 Yanga. Huku mechi ya pili Machi 8, 2015, Simba ikauwa kwa bao 1-0 Yanga, mfungaji alikuwa Emmanuel Okwi dakika ya 52.
2015/16
Septemba 26, 2015, Yanga 2-0 Simba, mabao yalipachikwa na Amissi Tambwe dakika ya 44 na Malimi Busungu dakika ya 79.
Kisha Februari 20, 2016, Yanga wakaichapa tena Simba kwa idadi hiyo ya mabao. Safari hii Mzimbabwe Donald Ngoma dakika ya 39 na Amissi Tambwe dakika ya 72 ndiyo waliingia kambani.
2016/17
Oktoba Mosi, 2016 mzigo uliisha kwa sare ya bao 1-1. Winga Shiza Kichuya ndiye aliyekuwa shujaa wa Simba akifunga bao dakika ya 87 na Amissi Tambwe dakika ya 26 kwa Yanga.
Februari 26, Simba 2-1 Yanga. Mrundi Laudit Mavugo akifunga dakika ya 66 na Shiza Kichuya dakika ya 81 kwa Simba, Simon Msuva dakika ya 5 kwa Yanga.
2017/18
Oktoba 28, Yanga 1-1 Simba.
Kwa Simba ni Shiza Kichuya dakika ya 58 na Obrey Chirwa dakika ya 60 kwa Yanga.
Aprili 29, Simba 1-0, bao lilipachikwa na Erasto Nyoni dakika ya 36.
2018/19
Septemba 30, Simba 0-0 Yanga, Februari 16, Yanga 0-1 Simba, Meddie Kagere dakika ya 72.
2019/20
Januari 4, 2020 Simba 2-2 Yanga wafungaji kwa Simba walikuwa ni Meddie Kagere 42 na Deo Kanda dk 46 huku kwa Yanga yakifungwa na Balama Mapinduzi dk ya 49 na Mohamed Issa dk 52.
Mghana Bernard Morrison alikata furaha ya Simba pale Machi 8, baada ya kufunga bao pekee kwa Yanga wakati wakishinda 1-0 mbele ya Simba. Morrison alifunga dakika ya 44.
Kwa rekodi hizi Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu Cedric Kaze kesho ina kazi ya kuendeleza pale ilipoishia msimu uliopita kwa kupata ushindi mbele ya Simba huku Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck ikiwa na hasira za kulipa kisasi cha kuchapwa mechi yao iliyopita.
Kuhusu mchezo huo, Kaze ameliambia Championi Ijumaa kuwa: “Natambua utakuwa mchezo mgumu ila hakuna namna ya kufanya kwa wachezaji wangu kupambana kusaka pointi tatu ndani ya uwanja.
“Wapinzani wangu Simba ninawatambua na ninajua ni timu bora lakini tupo tayari na ninawaamini wachezaji wangu,” alisema.
Sven wa Simba alisema: “Kupoteza mechi mbili mfululizo mbele ya Tanzania Prisons na Ruvu Shooting ni somo kwetu na sehemu ya mchezo ila tutapambana kupata ushindi kwenye mechi yetu dhidi ya Yanga.”
LUNYAMADZO MLYUKA, Dar es Salaam
